MGONJWA aliyelazwa wodi namba sita ya Jengo la Mwaisela katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) amenusurika kifo baada ya kujirusha kutoka ghorofa ya kwanza.
Aidha, uongozi wa MNH umeanika sababu ambayo kijana huyo (jina tunalihifadhi) ameeleza kuhusu kilichomsukuma kuchukua uamuzi huo mgumu wa kujirusha kutoka ghorofani.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi hospitalini hapo baada ya kijana huyo wa kiume (25) kukimbia kuelekea kwenye dirisha lililokuwa wazi na kujirusha.
Msemaji wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaeshi, akizungumza na Nipashe jana mchana, alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akieleza kuwa mgonjwa huyo alihisi kuna watu wanamfuata na kuamua kukimbia na kujirusha kwenda chini.
Alisema mgonjwa huyo anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata kichwani kutokana na tukio hilo.
"Jeraha lake si la kushonwa nyuzi, amesafishwa na kuwekewa dawa, yupo wodini anaendelea vizuri," alisema na kufafanua: "Wakati madaktari wanaendelea na kazi zao, alikimbia na kuelekea dirishani akidhani ni mlangoni na kujirusha kutoka gorofa ya kwanza alipokuwa amelazwa hadi chini."
Eligaeshi aliongeza kuwa wameagiza mgonjwa huyo afanyiwe kipimo cha CT Scan ili kujiridhisha kama kutakuwa na majeraha ya ndani aliyoyapata kutokana na tukio hilo nadra kutokea hospitalini hapo.
Alisema mgonjwa huyo ni wa rufaa kutoka katika Hospitali ya Amana na alipokewa na kulazwa Muhimbili juzi na tayari jopo la madaktari limeshamuona na kuchukuliwa vipimo vya awali.
Hata hivyo, Eligaeshi hakuwa tayari kueleza ugonjwa anaougua kijana huyo kiasi cha kulazwa katika hospitali hiyo kwa maelezo kwamba "ugonjwa ni siri ya mgonjwa".
"Kimaadili haitakiwi kuwekwa hadharani mpaka mhusika atakapokuwa tayari. Anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na ugonjwa wake uliosababishwa kulazwa hapa Muhimbili," alisema.
Eligaeshi aliongeza: "Tukio kama hilo lilishatokea kipindi cha miaka ya nyuma, kuna mgonjwa alijirusha na kuumia."