UBADHIRIFU wa kutisha unaohusisha mabilioni ya fedha, umefichuliwa kwenye Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ukihusisha uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni.
Wanaodaiwa kuhusika na utafunaji wa mabilioni hayo, walitumia mabadiliko mapya ya usajili wa vitambulisho, yaliyoigharimu serikali kupitia manunuzi yasiyo na tija huku wadanganyifu wakitumia mianya iliyopo kujinufaisha wenyewe kinyume na taratibu.
Kutokana na hali hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad, aliagiza wale vote waliohusika na ubadhirifu na udanganyifu wa mabilioni ya fedha, wachukulie hatua kali.
"Ukaguzi umejiridhisha kwamba, uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu na udanganyifu kwenye matumizi ya fedha katika mradi wa kuboresha vitambulisho vya taifa,"alisema.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonesha ubadhirifu katika eneo la usajili na utambuzi ambako Sh bilioni 1.2 zililipwa kwa huduma za bima kupitia dalali wa Bima M/s Aste Insurance Brokers Company Limited. Kiasi hicho kililipwa zaidi ya gharama halisi isivyostahili.
Huduma hizi zilipaswa kugharimu Sh milioni 450.2, lakini mamlaka ililipa Sh bilioni 1.7. CAG alibaini kuwa dalali huyo wa bima, alitumia akaunti za biashara katika kupokelea fedha za malipo ya bima ya Sh bilioni 1.7 badala ya akaunti ya amana isivyostahili.
Kwa hali hiyo, CAG amependekeza kampuni ya uwakala wa bima irejeshe Sh bilioni 1.2 zilizolipwa zaidi isivyostahili; na hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya Astery Ndege na kampuni hii kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kutoka mamlaka.
Ubadhirifu mwingine alioutaja ulikuwa ni manunuzi ya bima ya vifaa vya usajili na magari yaliyotumika katika mradi wa vitambulisho vya Taifa ya jumla ya Sh milioni 494, yaliyofanyika bila kukihusisha Kitengo cha Manunuzi.
CAG pia ameshauri hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watumishi waliohusika katika udanganyifu, uliobainishwa na kutozingatia sheria za manunuzi ya umma na kuisababishia Mamlaka gharama zisizo na tija sanjari na kuhakikisha kuwa wahusika wanafidia hasara iliyopatikana, kisha kuhakikisha udhibiti wa vifaa.
Uhakiki wa leja za mafuta, pia ulibaini kuwa lita 1,110 za mafuta ya dizeli yenye thamani Sh milioni 2.2 zilitumika kwa shughuli zisizo za Mamlaka.
Pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilikopa Sh milioni 455.3 kutoka NIDA kwa ununuzi wa magari manne mwaka 2014, ambazo hadi ukaguzi unafanyika Oktoba 2016 fedha hizo hazikuwa zimerejeshwa.
Uhakiki wa fomu zenye ‘Barcode’ zilizotengenezwa kupitia mpiga chapa binafsi M/s MFI Solution, ulibaini kuwa fomu 7,762,907 zenye thamani ya Sh bilioni 2.5 zilizopokelewa na mamlaka hazikutumika.
Kadhalika, ilibainika kuwa fomu 8,220,000 zenye thamani ya Sh milioni 519.6 zilizochapishwa tangu mwaka 2011/2012 hadi 2013/2014 hazikutumika; hivyo kutelekezwa katika stoo za TANITA.
“Hali hii ilitokana na mamlaka kutokuwa na Mpangokazi, hivyo kuingia hasara ya Sh milioni 932.8,” ilisema ripoti hiyo.
Matengenezo ya magari
Aidha, kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 mpaka 2015/2016, Mamlaka ilifanya matengenezo ya magari kupitia gereji binafsi yaliyogharimu Sh bilioni 1.3.
Nida pia ilifanya matengenezo yaliyogharimu Sh bilioni 1.1 yaliyofanyika na kulipwa na Mamlaka bila kufanyika ukaguzi unaothibitisha kuwapo kwa ubovu wa gari na mahitaji ya matengenezo husika.
Pia kulikuwa na matengenezo yaliyogharimu Sh milioni 197.2, yaliyofanyika na kulipiwa na Mamlaka bila kufanyika ukaguzi wa awali wala ukaguzi baada ya matengenezo.
Ripoti imeeleza kuwa ukaguzi ulibaini malipo ya Sh milioni 42.7 yalifanyika zaidi ya madai stahili kutokana na udanganyifu wa kuongeza tarakimu katika hati za madai na kutumiwa kwa hati moja ya madai zaidi ya mara moja katika malipo ya kuanzia mwaka 2012/2013 hadi 2015/2016.
Ajira za muda na za kudumu
NIDA imegundulika kuwa ilikiuka sheria katika ajira za muda na za kudumu, zilizofanywa na mamlaka kuanzia mwaka 2012 hadi 2015, ambapo vibarua 1,071 walipatikana kwa kupigiwa simu bila kutangaza mahali popote kinyume na Sera ya mamlaka hiyo. Ukaguzi ulibaini kuwa NIDA iliomba kupatiwa vibarua kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Chuo cha Utumishi wa Umma wapatao 415.
Lakini baada ya kupatiwa vibarua hao, mamlaka haikuwatumia na kubainisha kwamba wangetumiwa siku za baadaye. Ripoti ilifafanua kuwa mamlaka iliamua kuajiri vibarua wengine wapatao 882 bila kutangaza mahali popote, tofauti na watumishi 415 ambao walikwishapatiwa. Pia Septemba 2015 Mamlaka iliajiri watumishi 213 licha ya kibali cha kuajiri kutoka Utumishi kuisha tarehe Aprili 2015.
NIDA pia inatuhumiwa kufanya malipo Sh milioni 16.6 ya kiinua mgongo kwa vibarua, kinyume na mkataba wa ajira ya muda na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.
Ubadhirifu mwingine uligundulika kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na petroli, yaliyonunuliwa na mamlaka yenye thamani ya Sh bilioni 2.3, yaliyotolewa kwenye magari na majenereta, ambapo hayakuthibitika matumizi yake kutokana na sababu mbalimbali.
CAG pia amebaini upotevu wa vifaa vyenye Thamani ya Sh milioni 93.7 katika stoo ya mamlaka. Ukaguzi umebaini kuwa hakukuwa na taarifa rasmi kutoka kwa mtunza stoo juu ya upotevu huo, licha ya kufahamu kuhusu upotevu wa vifaa hivyo. Vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 991.4 havikutumika tangu kununuliwa kwake katika vipindi tofauti kuanzia Machi 2013 hadi Oktoba 2016.
Udanganyifu mwingine ulifanyika katika ushindanishi wa wazabuni katika ununuzi wa vifaa vya TEHAMA. Nida ilifanya manunuzi ya Ipad zenye thamani Sh milioni 63.4 zilizonunuliwa kutoka kwa M/s Elite computers baada ya kuonekana kukidhi vigezo vya ushindani na kupewa zabuni saba (7) tofauti. Lakini taarifa za wazabuni ambao waliainishwa kuwa washindani katika zabuni hii, M/s Prudent Enterprise na M/s Morex General Enterprise zilighushiwa; na wazabuni hawa hawakuhusishwa wala kutoa nukuu za bei.
Upangishaji nyumba Mamlaka ilitoa zabuni ya kuipangisha Ofisi ya Mamlaka kwa Mary Mwema kupitia barua ya maombi ya tarehe 06.05.2012 ambapo tangazo la zabuni husika ni la tarehe 25.05.2012 baada ya tarehe ya kuomba.
“Zabuni husika haikupitia Kitengo cha Manunuzi na haikuwa imeidhinishwa na Bodi ya Zabuni,” inasema ripoti hiyo.
Pia ripoti ilifafanua kuwa mzabuni wa upangishaji wa jengo la ofisi ya John Masenga haukujumuishwa kwenye mchakato wa tathmini ya kitaalamu licha ya kukidhi vigezo.