Kocha wa Mbeya City Kinna Phiri amewashutumu waamuzi wa bongo hususan waliochezesha mechi ya jana Jumamosi March 4, 2017 kwa kusema hawalisaidii soka la Tanzania.
Phiri ameilalamikia penati iliyotolewa dakika za lala salama akidai Mohamed Hussein wa Simba alijiangusha lakini mwamuzi akatoa mkwaju wa penati kwa Simba ambao ulikwamishwa wavuni na Shiza Kichuya na Simba kupata goli la pili la kusawazisha.
“Waamuzi wanatakiwa kujitahidi kuboresha viwango vyao, ni mara ya pili kwenye mechi yetu tunaadhibiwa kwa penati ambazo zina utata, Tuliopocheza na Prison walipewa penati kutokana na mtu kupiga mpira kwa kichwa lakini ikatolewa penati kwa madai kwamba aliushika mpira,” – Kinna Phiri.
“Hii inaashiria kwamba, waamuzi wanakuja uwanjani tayari wakiwa wanajua timu gani inatakiwa kunshinda kitu ambacho si kizuri kwa soka la Tanzania. Kwa upande wangu namna penati ilivyotolewa, nadhani haikustahili kuwa penati.”
“Sare kwa upande wetu haikupaswa kuwa kwa mtindo ule, tulipaswa kushinda mchezo dhidi ya Simba lakini maamuzi ya mwisho ni ya mwamuzi tunakubali sare lakini tulicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi.”
Mechi ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa kwenye uwanja wa taifa ilimalizika na kumuacha mwamuzi Ahmed Simba kwenye lawama baada ya kulikataa goli la Yanga lililofungwa kwa kichwa na Obrey Chirwa kisha mwamuzi huyo kumzawadia kadi ya njano akimtuhumu Chirwa kufunga kwa mkono.
Dakika chache baadae akamuonesha kadi ya njano iliyozaa kadi nyekundu, Yanga wakalalamika kwa bodi ya ligi na baadae kadi ya njano ya Chirwa ikafutwa na kumtoa kwenye kifungo cha kadi nyekundu.