Mtibwa Sugar wameilazimisha Yanga kutoka suluhu kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliopigwa leo Jumapili March 5, 2017 kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Yanga walikua wakihitaji ushindi kwa namna yoyote ili kurejea kwenye nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi baada ya jana Simba kupigwa stop na Mbeya City kufatia sare ya kufunga 2-2.
Yanga ikiwa bila wachezaji wake nyota kama Ngoma, Niyonzima, Tambwe, Kamusoko na Juma Abdul imejikuta iking’ang’aniwa na Mtibwa Sugar ambayo bado inatafuta ushindi wake wa kwanza tangu kuanza kwa mwaka 2017.
Matokeo ya suluhu kati ya Yanga na Mtibwa Sugar yanaifanya Yanga kuendelea kuwa nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi mbili. Yanga imeongeza pointi moja na kufikisha pointi 53 katika nafasi ya pili huku wapinzani wao wakiwa na pointi 55 katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi.
Tayari Simba na Yanga zimeshacheza mechi 24 na kusaliwa na mechi sita kabla ya ligi kufikia tamati.