SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 5 Machi 2017

T media news

Makonda: Nisemeni tu mwisho mtanyamaza

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kelele zinazoendelea dhidi yake ni dalili za mafanikio katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Makonda ameyasema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi katika tamasha la Twendezetu Kigamboni lililofanyika katika wilaya.

Amesema, mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni ya kufa au kupona.

“Mfahamu kuwa tunapambana kati ya mauti na uzima, kelele, mwangwi vinavyoendelea sasa ni dalili njema kwamba tunaendelea kunyooka,” amesema Makonda.

Makonda alisema Dar es Salaam ya sasa anaifananisha na chuma kilichopinda na sasa kiko katika hatua ya kunyooka hivyo lazima zitokee kelele nyingi kama ambavyo zinaendelea sasa.

“Huwezi kufanya kazi ya kunyoosha chuma bila kusikia mwangi, kelele na maumivu kwa sababu kazi ya kukomboa vijana dhidi ya dawa za kulevya si rahisi,” amesema Makonda.

Amesema katika kipindi hicho ambacho amekiita kuwa ni cha kulinyoosha Jiji la Dar es Salaam ni lazima kelele zisikike, uonekane moto unaoacha maumivu makali na baada ya hapo ije picha ya chuma kilichonyooka ambayo ndio picha ya Jiji la Dar es Salaam itakayokuwa imenyooka.

Amesema kelele hizo zitapita na mwisho lazima kufika ng’ambo ya pili pasipo na dawa za kulevya, kwenye taifa lililojengwa na uchumi imara.

Amelipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada zake za kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa ambapo alisema hivi sasa katika Jiji la Dar es Salaam dawa hizo zimepungua.

“Nitoe pongezi kwa Jeshi la Polisi dawa za kulevya zimepungua sasa Dar es Salaam na pia niwapongeze pia vijana ambao wanaendelea kutoa taarifa,” alisema Makonda.

Aliwaasa wananchi kushirikiana na Rais John Magufuli ambaye anafanya jitihada kuijenga Tanzania ya kesho iliyo bora. Kuhusu Kigamboni alisema anatarajia kuiona Kigamboni ikiwa mji wa mfano ambao haujaharibiwa na matendo yasiyofaa ikiwa ni pamoja na uhalifu na vijana walioharibika kutokana na matumizi ya dawa za kulevya badala yake kuwe na vijana wachapakazi.

“Watu watakapokuja Kigamboni wakute ni mji msafi, salama, uliopangika unaofaa kupumzika… mji ulio salama usio na uhalifu,” amesema Makonda.

Amewataka wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hashim Mgandilwa na viongozi wake katika kutimiza ndoto hiyo ya kuifanya Kigamboni tulivu na salama.

Amewaasa wazazi kuhakikisha wanafuatilia mienendo ya watoto wao kuhakikisha hawajiingizi katika matumizi ya dawa za kulevya na pia vijana kuchungana wao wenyewe.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Mgandilwa alisema lengo la tamasha hilo ni kuzitambulisha fursa zilizopo katika wilaya hiyo, kuwakutanisha vijana kupiga vita dawa za kulevya na pia kuiunga mkono serikali katika kufanya mazoezi.

Tamasha hilolilihudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Faustine Ndungulile Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Rahel Mhando na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.