RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Tundu Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, amesikitishwa na hatua ya Jeshi la Polisi – kitengo cha Bandari kuendelea kumshikilia Ramadhani Mussa Hamisi Ukwaju, bila kumfikisha mahakamani ama kumwachia kwa dhamana.
Ramadhani ndiye anayehusishwa na tukio la kusafirisha magari matatu ya kifahari aina ya Range Rover katika makontena ambayo taarifa zake zilionyesha mzigo huo ni nguo za mitumba, tukio lililofichuliwa na Rais Dk. John Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar e s Salaam takriban wiki moja iliyopita.
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na pia Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, aliweka bayana hayo jana, Machi 27, 2017. Kwa mujibu wa taarifa ya Lissu ambayo ‘tovuti’ hii imeinasa, Ramadhani amekuwa mahabusu kwa wiki kadhaa sasa.
“Nimetoka Polisi Bandari muda huu. Nilikwenda kumwona mtu aitwaye Ramadhani Mussa Hamisi Ukwaju ambaye yuko mahabusu ya Polisi Bandari tangu tarehe 4 ya mwezi huu. Ukwaju anatuhumiwa kuhusika na mzigo wa magari ya kifahari yaliyokamatwa na Bwana Mkubwa Rais siku chache zilizopita. Leo ni siku ya 23 yuko mahabusu. Hajapelekwa kwenye mahakama yoyote na hajashtakiwa kwa kosa lolote lile,” anaeleza Lissu
Anaendelea; “Suala lake limeshafika kwa DPP (Mwendesha Mashitaka) na kwa RPC Simon Sirro tangu siku kadhaa zilizopita lakini kila mkubwa anayehusika anaogopa kutoa maamuzi ya kumpeleka mahakamani au hata kumwachia kwa dhamana ya polisi.”
Kwa mujibu wa Lissu, hayo ndiyo madhara ya rais kuingilia majukumu ya kisheria yasiyomhusu. Anasisitiza; “Rais wetu anaweza kuwa Amiri Jeshi Mkuu lakini yeye sio askari polisi mwenye jukumu la kukamata wahalifu au kupeleleza makosa wanayotuhumiwa nayo.”
Anasema japokuwa ni Rais ndiye anayemteua DPP, lakini yeye si DPP na hana mamlaka ya kuamua nani apelekwe mahakamani na nani asipelekwe.
“Sasa inapotokea Rais anakwenda kwenye matukio ya uhalifu, kama ilivyokuwa kwenye suala la Ukwaju, anawafanya watendaji wanaohusika nayo washindwe kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.
“Katika mazingira ya sasa ya 'utumbuaji majipu', watumishi wa umma wanaogopa kufanya maamuzi kwa hofu ya kutumbuliwa majipu, hasa kwa masuala ambayo yameshafikishwa kwa Rais kwa njia extra-legal kama hili la Ukwaju. Matokeo yake haki za wananchi za kuwa huru zinakiukwa bila sababu za msingi.”
“Haya ni masuala ambayo TLS chini ya uongozi wangu inatakiwa kuyashughulikia. Hii ni sehemu ya agenda tutakayompelekea Rais na IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) na AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) pamoja na Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi tutakapoenda kuonana nao kama tulivyokwishawaomba. Kila mmoja wetu, mawakili na wasiokuwa mawakili tuyapigie kelele matumizi mabaya ya mamlaka ya kiupelelezi na ya kipolisi yanayopelekea haki za wananchi wetu kuvunjwa namna hii,” anasema Lissu na kuongeza kuwa kelele zitasaidia, ukimya ni sawa na kuyaunga mkono matendo hayo aliyoyaita mabaya.