HATUA ya Rais John Magufuli kumteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania imeibua utata kuhusu dhamira yake kwenye kufanya hivyo, Raia Mwema limeambiwa.
Tangu Uhuru wa Tanganyika, hakuna Rais aliyewahi kumteua mtu kuwa Kaimu Jaji Mkuu; baada ya Jaji Mkuu aliyekuwepo madarakani kumaliza muda wake wa utumishi kwenye mhimili huo wa dola.
Profesa Juma ambaye anachukuliwa kama mgeni kwenye mhimili huo, aliteuliwa na Rais Magufuli mapema mwaka huu kuwa Kaimu Jaji Mkuu akichukuwa nafasi ya Chande Othman aliyefikia umri wa kustaafu.
Mazungumzo baina ya gazeti hili na wandani wa Mahakama hapa nchini yameeleza hali hiyo kuleta utata kwa vile tukio hilo halijawahi kutokea na halina maelezo ya maana kulitetea.
“Sikiliza, hii nchi haijawahi kuwa na Kaimu Jaji Mkuu aliyeapishwa wakati Jaji Mkuu akiwa amestaafu. Hii ni mara ya kwanza na kwa kweli imeleta mkanganyiko mkubwa.
“ Kaimu Jaji Mkuu anaweza kuapishwa wakati Jaji Mkuu akiwa kwenye safari ya muda mrefu nje ya nchi au akiwa na tatizo linaloweza kuathiri utendaji kazi wake. Hapo Kaimu anaweza kuapishwa lakini si kwa ilivyo sasa. Jaji Mkuu kastaafu sasa Rais anateua Kaimu wa nini?” alihoji mmoja wa majaji mashuhuri nchini aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa majina yake.
Jaji huyo alisema mtu akiwa anakaimu nafasi yoyote anakuwa hajiamini na hawezi kuchukua uamuzi mzito kwa sababu hajui kama atamfurahisha aliyemteua au la.
“Kama Rais alikuwa anamtaka Profesa Juma, angemteua tu kuwa Jaji Mkuu, hii kaimu haina maana sana. Imeleta mkanganyiko na utata tu,” alisema Jaji huyo.
Ingawa baadhi ya wanaharakati kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii wameenda mbali kiasi cha kusema kuna uvunjwaji wa Katiba kwenye uteuzi huo wa Kaimu Jaji Mkuu, Raia Mwema limebaini hakuna uvunjwaji wa Katiba uliofanyika kwenye jambo hilo.
Ibara ya 118 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toleo la mwaka 197, imeeleza kwa kirefu kuhusu nafasi hiyo ya Jaji Mkuu kama ifuatavyo:-
“118.-(1) Kutakuwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani
(ambaye katika ibara zifuatazo kwenye Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Jaji Mkuu" na Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani wasiopungua wawili, isipokuwa kwamba kikao maalumu cha Mahakama nzima kitakuwa kamili kikiwa na Majaji wa Rufani wasiopungua watano.
(2) Jaji Mkuu atateuliwa na Rais na atakuwa ndiye Kiongozi wa Mahakama ya Rufani na pia Mkuu wa Idara ya Mahakama kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 116 ya Katiba hii.
“(3) Majaji wengineo wa Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais, baada ya kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka miongoni mwa watu ambao wanaweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyoelezwa katika ibara ya 109 ya Katiba hii au kutoka miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa
kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa Sheria zinazotumika Zanzibar.
“(4) Iwapo itatokea kwamba:-
(a) Kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi; au
(b) Jaji Mkuu hayupo Tanzania; au
(c) Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi yake kwasababu yoyote na Rais akiona kuwa kwa muda watukio lolote kati ya hayo matatu inafaa kumteua Kaimu Jaji Mkuu, basi Rais aweza kumteua Kaimu Jaji Mkuu kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kustahili kuteuliwa kuwa Majaji wa Mhakama ya Rufani.
“Na huyo huyo Kaimu Jaji Mkuu atatekeleza kazi za Jaji Mkuu mpaka atakapoteuliwa Jaji Mkuu au mpaka Jaji Mkuu mwingine ambaye hakuwapo Tanzania au alikuwa hamudu kazi zake atakaporejea kazini.”
Kwa mujibu wa vifungu hivyo vya Katiba, Rais anaweza kuteua Kaimu Jaji Mkuu endapo “Kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi”; lakini haijafafanua uwazi upi kwani inaweza kuwa kwa sababu ya kifo, kustaafu, kusafiri, kuumwa au sababu nyingine yoyote inayokubalika.
Ukaimu wa Profesa Juma
Baadhi ya wandani hao wa Mahakama, wameliambia gazeti hili ingawa imekuwa ni kawaida kwa majaji kukaimu Ujaji Mkuu, mara nyingi wanaokaimu huendelea kutumia ofisi zao zilezile na magari yaleyale, jambo ambalo ni tofauti na sasa.
Raia Mwema limeelezwa kwamba Profesa Juma anatumia gari la Jaji Mkuu, anafanya kazi kwenye ofisi ya Jaji Mkuu na kutendewa kama Jaji Mkuu kamili, ilhali wadhifa wake huo haujathibitishwa.
Wakati wa Jaji Mkuu Francis Nyalali, Raia Mwema limeelezwa, mara kadhaa aliwahi kutibiwa nje ya nchi na nafasi yake kukaimiwa na Jaji Augustino Ramadhani, lakini hakuwahi kutumia gari wala ofisi ya Jaji Mkuu.
Ilikuwa hivyo hivyo kwa Jaji Eusebia Munuo ambaye aliwahi kukaimu nafasi ya Chande wakati alipokuwa nje ya nchi kwa muda mrefu lakini hakuwahi kutumia ofisi ya Jaji Mkuu wala gari lake.
“ Kwa mujibu wa Sheria za Utumishi, muda wa kukaimu nafasi ni miezi sita. Sasa tunasubiri kwa hamu baada ya kupita kwa miezi hiyo sita nini kitafuata.
“ Je, Rais Magufuli atamuita tena Jaji Juma kwa ajili ya kumuapisha kuwa Jaji Mkuu? Kama hatamuapisha, atatoa sababu za kutomuapisha? Je, watu wakisema amemtoa kwa sababu alikataa kuburuzwa itakuwaje?” Raia Mwema limeambiwa.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu suala hili, Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, alisema hatua ya Rais Magufuli kuteua Kaimu Jaji Mkuu ni dharau kubwa kwa majaji wa Tanzania.
Alisema kitendo cha Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu wakati kulikuwa na fursa ya kuteua Jaji Mkuu kamili kinatoa picha mbili kubwa; moja kwamba hakuwa tayari kwa uteuzi huo na pili hakuna majaji wenye sifa ya kuchukua wadhifa huo.
“Je, Rais anataka kuonyesha kwamba nchi hii haina majaji wenye uwezo wa kushika wadhifa huo kiasi kwamba ateue Kaimu Jaji Mkuu? Kwangu, naichukulia hii kuwa ni dharau kwa majaji wetu.
“ Mimi nasema Rais hajavunja sheria yoyote kwa kuteua Kaimu Jaji Mkuu lakini kinachogomba hapa ni picha anayoionyesha kwa mhimili huu. Kinachogomba ni dhamiri yake kwenye Idara ya Mahakama,” alisema Lissu.
Lissu alisema kazi iliyopo sasa kwa wanasheria, asasi za kijamii na vyombo vya habari ni kumkumbusha Rais kwa nguvu zote kwamba Idara ya Mahakama inatakiwa kuongozwa na Jaji Mkuu mwenye mamlaka kamili na si ya kukaimu.
“Na nyie mjiulize, Jaji Mkuu amestaafu, Kaimu Jaji Mkuu wa nini? Kaimu inakubalika tu wakati mhusika anapokuwa nje ya nchi au kwa sababu nyingine kama zilivyoelezwa kwenye Katiba. Hili la kuteua Kaimu wakati Jaji Mkuu amestaafu ndiyo kalileta Magufuli,” alisema.
Jaji Ibrahim Hamis Juma ni msomi mbobezi wa masuala ya sheria akiwa amewahi kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Aliapishwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu Januari mwaka huu na kwa mara ya kwanza aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2008.
Credit - Raia Mwema