SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 20 Machi 2017

T media news

Kauli ya Rais Magufuli kuhusu RC Makonda “kusemwa” mitandaoni?


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Leo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuendelea kuchapa kazi na kutokusikiliza maneno ya watu ya kuvunja moyo na udaku unaoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza katika sherehe za kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya barabara Ubungo, Rais amesema kuwa amefurahishwa sana na mradi uliotolewa na Benki ya Dunia na anatamani ukamilike hata kabla ya muda uliopangwa wa miezi 30.
Akizungumzia suala lililojadiliwa kwa ukubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu RC Makonda, amewataka wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuacha kutumia muda mwingi katika habari za udaku ambazo zinawapotezea muda na hazisaidii jambo lolote au kumaliza matatizo ya wananchi wa Tanzania.
Suala hilo la Makonda limeibuka baada ya kiongozi huyo kuvamia ofisi za Clouds Media Group usiku Machi 17 akiwa ameongozana na Askari wenye bunduki akiwashinikiza kurusha hewani kipindi alichokuwa amewaambia warekodi.
“Watu wa Dar es salaam tumejiendekeza sana kwenye udaku ambao hausaidii maendeleo. Udaku ambao hautuletei maji, hautuletei mchicha na wala hautuondolei foleni ya Dar. Watanzania mjue kampeni zimeshakwisha na mimi ndiye Rais hivyo hata mtu alie , ugaregare lakini rais ni mimi John Pombe Magufuli na kwangu ni kazi tu.”
Rais Magufuli amesema kuwa mambo yasiyo na msingi yanachukua muda wetu mwingi kitu ambacho hakisaidii maendeleo.
“Vitu ambavyo havina msingi vinachukua muda wetu mwingi sana. Mara unapost hiki mara uweke kile. Kuna wengine mmefikia hata hatua ya kunipangia cha kufanya. Nasema mimi ukinipangia ndio umeharibu. Mimi ni Rais ninayejiamini. Nadhani mmenielewa.”
Kuhusu baadhi ya watu kushinikiza kupitia mitandao ya kijamii kuwa Paul Makonda ajiuzulu, Rais Magufuli alisema, “Kuandikwa kwenye mitandao hata miimi ninaandikwa, kwa hiyo nijiuzulu? Kuandikwa kwangu mimi siyo tija bali kuchapa kazi. Kwahiyo Makonda wewe chapa kazi.”
“Mimi sionyeshwi njia na mtu. Njia ya kupita tayari nilishaonyeshwa na ilani ya chama changu. Mimi ni rais ninayejiamini, na mimi ndiyo ninapanga kiongozi gani awe sehemu gani”
Akimaliza kuhutubia umati wa wananchi waliojitokeza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amewataka wakazi wa Ubungo kulinda miundombinu na vifaa vitakavyotumika katika ujenzi huo. Lakini pia amemsihi Waziri wa Ujenzi, Prof. Mabarawa kuhakikisha kuwa wakazi wa Ubungo ndio wanakakuwa wa kwanza  kunufaika na mradi huo.