WINGA wa timu ya Tenerife inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Hispania, Farid Musa amesema anashukuru sana sapoti anayopewa na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye amekuwa akimtaka kuwa mvumilivu katika maisha ya soka la kimataifa la sivyo hatofika kokote.
Farid ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Stars waliocheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Botswana juzi Jumamosi, licha ya kutokea benchi alionesha kiwango cha juu kwa dakika chache alizocheza kipindi cha pili.
Shaffihdauda.co.tz ilipiga story na Faridi Musa ambaye alisema “Mara kadhaa Samatta nimekuwa nikiwasiliana naye na kunisisitiza kuendelea kuwa mvumilivu kwakuwa hakuna kitu kinachopatikana bila kukitolea jasho kwa wakati huu unapowaza kufanikiwa kama Cristiano Ronaldo ama Lione Messi.”
“Samata amenisihi sana niwe mvumilivu kwani anajua ugumu wa soka la Ulaya, lina mambo mengi na ili ufanikiwe jitihada na uvumilivu wa hali ya juu unahitajika,” alisema Farid.
Farid ambaye bado hajaanza kucheza kikosi cha kwanza katika klabu hiyo kutokana na kutokuwa na utimamu wa mwili akiwa kwenye kikosi cha pili alisema anakubaliana moja kwa moja na Samatta kuwa uvumilivu unahitajika ili kufanikiwa.