SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 3 Februari 2017

T media news

WAZIRI WA ZAMANI WA CCM ATISHIA KUZIMA MITAMBO YA MAJI

MBUNGE wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) ametishia kuwa endapo wananchi wake hawatopata maji kutoka chanzo cha maji cha Ihelele kama walivyoahidiwa na serikali, ataongozana na wananchi hao kwenda kuzima mitambo ya maji katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, chanzo hicho cha maji kwa sasa kinazalisha maji yanayopelekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Shinyanga na Kahama kupitia Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Kahama na Shinyanga (Kashuwasa).

Akiuliza swali la nyongeza bungeni Dodoma mbunge huyo alisema tangu serikali iwaahidi kuwa jimbo hilo la Misungwi litapata maji kupitia mradi huo wa maji wa Ihelele hadi sasa maji hayo hayatoki wakati maeneo mengine yanapata.

“Naibu Spika nasema wazi kuwa nitaongozana na wananchi wa jimbo langu kwenda kuuzima ule mtambo wa maji Ihelele kama maji haya yataendelea kutotoka kwenye maeneo yetu,” alisema Kitwanga ambaye aliposimama kuuliza swali hilo alishangiliwa sana na wabunge wenzake.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alimtaka mbunge huyo asiandamane na wananchi wake, kwani kilichokwamisha maji hayo yasifike jimboni kwake ni uhaba wa fedha za kuunganisha bomba la maji hadi eneo hilo ambapo zinahitajika takribani Sh bilioni nne.