Waziri wa Sheria na Katiba Dkt. Harrison Mwakyembe, amepongeza jitihada za Rais Magufuli za kupambana na dawa za kulevya huku akisimulia alivyoshindwa vita hiyo wakati alipokuwa Wazri wa Uchukuzi, hususan katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam
Amesema alipata taarifa za kichunguzi kuhusu jinsi dawa za kulevya zinavyopitishwa katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, na akaamua kutangaza vita akisaidiana na mtu ambaye hajamuweka wazi, lakini mwisho mtu huyo aliyekuwa akiongoza vita hiyo, aliishia kufungwa gerezani mpaka leo.
Mwakyembe amesema hata baada ya yeye kutumia nguvu zake kumtoa gerezani ameshindwa, jambo ambalo linaonesha kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya ni ngumu kuliko kawaida, huku akionesha matumaini kuwa katika awamu hii, serikali itashinda.
Dk. Mwakyembe amezungumza hayo jijini Dar es Salaam, alipokutana na wahadhiri na wanafunzi kutoka Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa lengo la kupokea mapendekezo ya kanuni ya kusimamia sheria mpya ya msaada wa kupata msaada wa kisheria iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni.