SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 4 Februari 2017

T media news

Waturuki Kujenga Reli ya Kisasa.......Treni Itatumia Saa 1;30 Kutoka Dar hadi Moro. Dar Hadi Mwanza ni Masaa 7 tu

Serikali ya Tanzania na kampuni za ujenzi za Uturuki na Ureno, zimesaini mkataba wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.21 (Sh trilioni 2.66).

Kati ya fedha hizo, dola za Marekani bilioni 1.21 (Sh trilioni 2.2) ndiyo gharama halisi ya ujenzi wa kipande hicho na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni dola milioni 1.85 (Sh bilioni 406).

Mradi huo unaotarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili na nusu, utaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili barani Afrika yenye reli kama hiyo ambayo inaweza kupitisha treni ya umeme inayotembea kwa mwendo wa kasi.

Akizungumza kabla ya kutilia saini mkataba huo jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema kwa sasa barani Afrika, Morocco ndiyo yenye reli kama hiyo inayopitisha treni inayotembea kasi ya kilomita 200 kwa saa.

Kukamilika kwa kipande cha reli ya Dar es Salaam mpaka Morogoro, treni inayotembea kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa itaweza kupita.

Profesa Mbarawa alisema hali hiyo itafanya safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kuwa saa 1:30.

Kukamilika kwa awamu ya pili ya reli hiyo kutoka Morogoro mpaka Dodoma kutaifanya safari ya treni hiyo ya umeme kutoka Dar es Salaam kwenda makao makuu ya nchi kwa kutumia saa 2:30 huku kitakapomalizika kipande cha Dar es Salaam mpaka Mwanza, kutaifanya treni hiyo kusafiri kutoka Dar es Salaam mpaka mkoa huo wa Kanda ya Ziwa kwa saa 7:30.

Kampuni zilizotia saini ujenzi wa reli hiyo ni Yapi Merkenzi Instant Ve Sanayi A.S ya Uturuki ambayo imeungana na Mota-Engil, Engenharia E and Construcao S.A ya Ureno.

Awamu ya kwanza ya reli hiyo kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro itakuwa na urefu wa kilomita 300 kati yake kilomita 205 ni njia kuu na 95 ni njia za kupishania treni.

Ujenzi huo utahusisha pia uzio wa usalama kutokana na reli hiyo kutumia umeme pamoja na ujenzi wa vivuko kwa watu na wanyama.

Profesa Mbarawa alisema: “Wakati tunafikiria ujenzi wa reli hii tuliwatuma vijana Kenya, Ethiopia na Nigeria kuangalia namna ambavyo wenzetu wamefanikiwa, tulilenga kuepuka makosa ambayo wenzetu waliyafanya ili tusiyarudie.

“Tuligundua nchi hizi treni yao inakwenda kilomita 120 kwa saa, tukajiuliza kwanini tusipate inayokwenda 160? Sasa tumepata inayokwenda kasi zaidi. Ya Kenya na Nigeria zinatumia mafuta, tukaenda Ethiopia tukakuta wao wanatumia umeme, tukaona kwanini na sisi tusije na inayotumia umeme? Sasa tumefanikiwa.”

Alisema reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani 35 kwa excel moja, ikilinganishwa na sasa ambapo reli ya zamani (meter gauge) ina uwezo wa kubeba tani 14 kwa excel moja.

Reli hiyo itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka kutoka tani milioni tano za sasa, hivyo kuifanya kuwa daraja la uchumi wa nchi kwa kuiunganisha na nchi za jirani ambazo hazina bandari.

“Tumeamua kufanya mradi huu kwa kasi na kuzingatia kiwango cha ubora wa reli yenyewe lakini pia gharama za ujenzi. Usafiri wa reli ni nafuu na inabeba mizigo mingi,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema itakapokamilika reli hiyo, itarahisisha usafiri ambapo mtu anaweza kuishi Dodoma au Morogoro na akafanya kazi Dar es Salaam.

Alisema gharama ya ujenzi huo inategemewa kushuka kwa eneo la kuanzia Morogoro hadi Mwanza kwani eneo hilo si la mwinuko kama ilivyo kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro.

Aliongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, Serikali itaongeza fedha za ujenzi wa reli hiyo ikiwa ni pamoja na kuomba mikopo kutoka kwa wahisani ili kuhakikisha wanaiunganisha Tanzania na kuifanya kuwa karibu zaidi tofauti na ilivyo sasa.

Alisema jumla ya kampuni 40 ziliomba zabuni ya kujenga reli hiyo lakini YAPI ya Uturuki inayoshirikiana na Mota ndiyo iliyorudisha zabuni.

Akizungumzia kuhusu kampuni za China kutopewa zabuni ya ujenzi wa reli hiyo alisema ni kwasababu hazikurudisha zabuni zao.

Wakati huo huo Waziri Mbarawa alisema tayari Serikali imetangaza zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kuanzia Morogoro hadi Makutupora kilomita 336, Makutupora hadi Tabora 294, Tabora hadi Isaka 133 na Isaka hadi Mwanza 248.

“Tunaikaribisha kampuni yoyote inayotaka kujenga na hakuna kampuni tutakayoionea ila uwezo wa kampuni na gharama za ujenzi zitaangaliwa,” alisema Waziri Mbarawa.

Akizungumza katika utilianaji saini huo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Profesa Norman King, alisema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo ni kutimia kwa ndoto za Rais Dk. John Magufuli za kuona Tanzania inakamilisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa.

“Pamoja na kuonekana kwa wengi tumechelewa lakini kuchelewa huku ni kuzuri kwa sababu tumeua ndege wawili kwa jiwe moja kwa kupata treni inayokwenda kasi na ya umeme,” alisema King.