SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 20 Februari 2017

T media news

Wanasheria wa CHADEMA Wamtaka Mbowe Asijisalimishe Polisi

Wanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamesema wamemshauri Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe, asiende kuripoti polisi leo.

Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, amesema Mbowe hatakwenda kuripoti polisi leo kwa sababu amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam na inaanza kusikilizwa Februari 21 mwaka huu.

“Mbowe haendi polisi, tumemshauri asiende kwa sababu kesi yake inaanza kusikilizwa Jumanne (kesho).

“Kama wanamhitaji, waje keshokutwa (kesho) Mahakama Kuu, watampata hapo,”alisema Mallya.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema yuko Mwanza na hajawasiliana na Mbowe.

“Hapa niko Mwanza sijawasiliana na mwenyekiti, lakini kama nikiwasiliana naye, nitamshauri asiende huko polisi.

“Kwa hiyo, naweza kusema kilichofanywa na Kamishna Sirro si wito wa kipolisi bali ni siasa kama ambavyo alifanya Makonda kwa kutangaza majina ya watu hadharani.

“Wito wa polisi huwa ni wa kimaandishi, hawajamwandikia barua, hawajampigia simu.

“Hawa maafande wana namba zetu za simu sisi kama mawakili wa chama, kama wanamhitaji Mbowe kwanini wasitupigie simu mpaka watangaze kwenye vyombo vya habari,”alihoji Lissu.

Alipoulizwa kama Mbowe atakamatwa wakati wowote kuanzia sasa, Lissu alisema watalazimika kulishtaki mahakamani Jeshi la Polisi kwa kitendo hicho.

“Hatuwezi kukubali utaratibu huu, waache kufanya siasa, wakimhitaji mwenyekiti wetu wamwandikie barua,”alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitaja majina 65 ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwamo Mbowe.

Pamoja na kutaja majina hayo, Makonda aliwaagiza watuhumiwa hao kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma hizo.

Februari 10 mwaka huu, akiwa mjini Dodoma, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alizungumza na waandishi wa habari na kusema hajawahi kujihusisha kwa namna yoyote na biashara ya dawa za kulevya na pia hatakwenda polisi kuhojiwa kama alivyoagizwa na Makonda.

Hata hivyo, alisema atakwenda polisi, kama jeshi hilo litafuata taratibu za kumuita kwa mujibu wa sheria.

“Siwezi kwenda polisi kwa wito wa Makonda kwa sababu hana mamlaka hiyo kisheria. Kama polisi wananihitaji, waniite kwa kufuata utaratibu, nitakwenda kwa sababu mimi siogopi kwenda polisi,”alisema Mbowe.

Wakati Mbowe akisema hayo, juzi Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema Jeshi la Polisi linamtafuta Mbowe na kwamba limeshindwa kumpata kwa sababu amezima simu.

Kutokana na hali hiyo, Kamanda Sirro alitoa saa 48 kwa Mbowe kuripoti polisi na endapo hatafanya hivyo atatafutwa kwa namna ambayo jeshi hilo litaona inafaa.

 “Jumatatu (leo) asiporipoti kutakuwa hakuna namna ya kulizuia tena Jeshi la Polisi kutafuta namna ya kumhoji.

 “Mbaya zaidi juzi tumejitahidi kumtafuta hapatikani, tulikwenda nyumbani kwake hakupatikana, tulikwenda mahali anakoishi sasa, pia hakupatikana,”alisema Sirro