SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 20 Februari 2017

T media news

UTAFITI: Bangi Inaharibu Ubongo

Wakati baadhi ya nchi zimeanza kuhalalisha matumizi ya bangi, utafiti mpya umegundua kuwa matumizi ya bangi yanaharibu ubongo.

Kwa mujibu wa jarida la sayansi la livescience, katika utafiti uliofanyika katika chuo kikuu cha Brown katika kisiwa cha Rhode, watafiti walitumia pia kisa cha mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 52 ambaye alikuwa mraibu wa matumizi ya bangi kwa zaidi ya miongo miwili. Mwanaume huyu alivuta bangi na kupoteza mtazamo wa mambo katika uhalisia, na hatimaye akajirusha barabarani akagongwa na gari na kupoteza maisha. Watafiti waliuchunguza ubongo wa mtu huyo na kugundua uharibifu mkubwa wa ogani hiyo muhimu uliosababishwa na uvutaji bangi wa muda mrefu.

"Looh, tulipouchunguza ubongo wake hakika ulikuwa umeharibika vibaya sana kutokana na uvutaji wa bangi" alisema Bibi, Dr Suzzane M. de la Monte ambaye ni profesa wa kitengo cha upasuaji wa mishipa ya fahamu kutoka chuo hicho.

Watafiti hao walisema hawakuelewa kwa usahihi ni kiasi gani hasa cha bangi alichotumia mtu huyo kabla ya kifo chake, lakini vipimo vya damu vilionyesha kuwepo kwa kiasi kikubwa cha kemikali zilizo katika mmea wa bangi na ziletazo madhara.

Watafiti walisema pia kuwa, huu ni uthibitisho ambao unaonyesha jinsi watu wanaotumia bangi kwa namna mbalimbali wanavyoweza kupata madhara. "Tuna wasiwasi sana kwa wale walio wadogo na vijana ambao bado wanakua" alisema profesa huyo. Ubongo wa watoto na vijana wanaokua, uko katika hatari zaidi ya kuharibiwa na kemikali hizi zitokanazo na bangi.

Katika utafiti mwingine uliofanyika katika chuo cha King's huko London, ulionyesha kuwa matumizi ya  kiasi kikubwa cha bangi kutokana na jamii mbalimbali za mmea wa bangi, husababisha uharibifu wa sehemu ya ubongo ijulikanayo kitaalam kama corpus callosum, sehemu ambayo inahusika na usafirishaji wa taarifa kati ya upande wa kushoto na upande wa kulia wa ubongo. Hii inaongeza hatari ya kupata magonjwa ya akili na mtumiaji kuwa mwendawazimu ambapo dalili zake ni kuwa mgonjwa atakuwa anaona mambo kinyume na uhalisia.

Wanasayansi wamegundua pia ,kiwango cha kemikali ijulikanayo kama Delta9- tetrahydrocarnnabinol(THC) katika bangi, ni kikubwa kuliko miaka kumi iliyopita.

Wanasayansi hao kwa kutumia technolojia ya upigaji picha za ubongo kwa wagonjwa walioathirika na uraibu wa bangi wakilinganisha na wale waliojitolea waliokuwa na afya njema, waligundua uharibufu mkubwa wa ubongo kwa wale wanaotumia bangi kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na wale wanaotumia kiasi kidogo na wale wasiotumia kabisa.

Watafiti hao walihitimisha kwa kusema kuwa "kuna uhitaji wa haraka sana na wa dharura" wa kutoa elimu ya afya ili kukiepusha kizazi hiki na madhara makubwa yatokanayo na utumizi sugu wa madawa haya hatari ya kulevya.