Mchekeshaji maarufu nchini, Emmanuel Mathias aka MC Pilipili ambaye pia alikuwa mtangazaji wa Times FM , amedai ameamua kuachana na kazi hiyo ili akaze zaidi kwenye uchekeshaji.
Akiongea na Bongo5 wiki hii, MC Pilipili alidai kazi ya utangazaji ilikuwa inabana ratiba zake kwa kiasi kikubwa hali ambayo ilikuwa inamfanya ashindwe kufanya baadhi ya vitu.
“Nilianza kwa kuacha kazi yangu ya kwanza ya ualimu ili kuwa mchekeshaji, leo hii tena naacha kutangaza ili kuongeza nguvu kwenye uchekeshaji,” alisema MC Pilipili. “Kazi ya redio inahitaji muda sana, sasa kuna wakati nataka kufanya jambo fulani kuhusu uchekeshaji nakuta ratiba zinaingiliana, kwahiyo nimeona bora niendelee na kazi yangu ya uchekeshaji,”
Aliongeza, “Kwahiyo sasa hivi kilichobaki ni kazi tu, tayari nimeshaingia darasani kujifunza lugha ya kingereza, mungu amesaidia sasa hivi niko vizuri ingawa bado naendelea na stage ya pili, yote haya nafanya kwajili ya kumpeleka MC Pilipili kimataifa zaidi,”
Mchekeshaji huyo ni mmoja kati ya wachekeshaji vijana ambao wanamafanikio makubwa kwenye tasnia hiyo.