Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa yupo tayari kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Mhe. Rais Museveni amesema hayo jana tarehe 26 Februari, 2017 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakati akiagana na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli baada ya kumaliza ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku 2 hapa nchini na kurejea Uganda.
“Tulikuwa na mazungumzo mazuri na Mhe. Rais Magufuli, tumejadili mambo mengi hususani kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta, tumekubaliana na Mhe. Rais mambo mengi, na sasa tutakwenda kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo” alisema Mhe. Rais Museveni.
Mhe. Rais Museveni aliwasili hapa nchini juzi asubuhi tarehe 25 Februari, 2017 ambapo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli na jana alitembelea viwanda viwili vinavyomilikiwa na kampuni ya mfanyabiashara wa Tanzania Bw. Said Salim Bakhresa ambavyo ni kiwanda cha uzalishaji wa unga wa ngano kilichopo Buguruni na kiwanda cha uzalishaji wa juisi kilichopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam.
Licha ya kuwekeza nchini Uganda Mfanyabiashara huyo pia amekuwa akipeleka bidhaa zake kwa wingi nchini Uganda.
Pamoja na Mhe. Rais Magufuli viongozi wengine waliokuwepo wakati wa kumuaga Mhe. Rais Museveni ni pamoja Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.