Rais wa Syria, Bashar al Assad ametetea mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kuzuia wahamiaji na wakimbizi kutoka mataifa saba yenye imani kali ya Kiislamu.
Assad amesema mpango wa Trump sio kuwazuia raia wa Syria kuingia kwenye taifa hilo kubwa la Marekani ila ni kupambana na magaidi ambao wanahatarisha usalama wa maeneo mengi duniani kwa sasa.“Ni dhidi ya magaidi ambao wanaweza kuingia kwa kujipenyeza kupitia baadhi ya wahamiaji, na hilo limeshatokea, lilitokea Ulaya, nchi kama Ujerumani,” alisema Assad wakati akifanyiwa mahojiano na kituo cha redio cha Europe 1 na kituo cha runinga cha TF1.
“Nadhani malengo ya Trump ni kuzuia watu wote ambao wanakwenda, sio kuzuia watu ambao wanatokea Syria,” amalizia Rais huyo wa Syria.
Hata hivyo mpango wa Trump kuwazuia wahamiaji na wakimbizi wasiingie Marekani tayari unaonekana kukwama baada ya mahakama kutengua agizo hilo na kuruhusu wahamiaji na wakimbizi kuendelea kuingia kama kawaida japo tayari Trump ameshasema atatafuta njia mbadala ya kuwazuia wasiingie Marekani.