SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 15 Februari 2017

T media news

Marekani yatakiwa kuomba msamaha

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, ameitaka marekani kuomba msamaha na kuondoa vikwazo dhidi ya makamu wake, Tareck El Aissami.

Anashutumiwa na marekani kwa kuhusika na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Bw Maduro amesema anamuunga mkono kwa dhati Bw El Aissami ambaye ametaja hatua ya Washington kama uchokozi wa kibeberu.


Wizara ya fedha Marekani ilisema Tareck el-Aissami ni mlanguzi mkuu wa dawa za kulevya na amekuwa akifanya kazi na walanguzi Mexico na Colombia kusafirisha mihadarati hadi Marekani.

Vikwazo alivyowekewa vinahusisha kuzuiwa kwa mali yake Marekani na pia amepigwa marufuku kuzuru taifa hilo.

Amekuwa akitangazwa kama mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika chama tawala.

Bw Maduro ana imani naye sana na amempa baadhi ya majukumu ambayo kawaida hutekelezwa na rais pekee, mfano kuamua bajeti za wizara mbalimbali pamoja na kutaifishwa kwa kampuni za kibinafsi.

Marekani imesema amekuwa akilipwa na mlanguzi mkuu wa dawa Venezuela Walid Makled kulinda mihadarati yake inapokuwa inasafirishwa.

"Hawataweza kabisa kuvunja azma yetu ya kusalia tukiwa huru daima," Bw Aissamu amesema.

Marekani pia imewekea vikwazo mfanyabiashara mashuhuri Venezuela Samark Lopez.

Bw Lopez baadaye alitoa taarifa na kusema hahusiki kwa vyovyote katika ulanguzi wa dawa za kulevya.

Bw Aissami ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa Venezuela kuwahi kuwekewa vikwazo na Marekani.

Mataifa hayo mawili hayajakuwa na uhusiano wa kibalozi tangu 2010.

Wataalamu wa kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya wamekuwa kwa muda sasa wakisema wanaamini shehena kubwa ya kokeni kutoka Colombia hupitishiwa Venezuela kabla ya kuelekezwa Ulaya na Marekani.