Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema kwa sasa viongozi madalali wanaouza viongozi ndani ya chama hicho hawatakiwi, huku akiwataka watafute kazi nyingine za kufanya.
Kutokana na hali hiyo amesema sasa wamejipanga kuhakikisha CCM inaendelea kutawala maisha yote huku akiwataka wenyeviti wa kata, wilaya na mikoa kutokuwa sehemu ya malalamiko na badala yake wawe sehemu ya kusimamia Serikali kama anavyofanya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya CCM yaliyofanyika katika ukumbi wa Dodoma Convention Centre, ambao unamilikiwa na chama hicho, ambapo Kinana awalitaka viongozi wa chama hicho kuacha kuwa walalamikaji na badala yake wawe sehemu ya kuisimamia Serikali katika kutimiza wajibu wake.
“Sasa hatutaki kuwa na viongozi madalali ndani ya chama, kwa hiyo kama wapo wajitafakari wenyewe. Ndiyo maana hata sisi tumekubaliana maadhimisho sio sherehe lazima tuachane na tabia za sherehe ukisema sherehe itabidi pia mlipane na posho jambo ambalo halikubaliki,’’ alisema Kinana.
Akielezea sababu za kuendelea kushinda kwa chama hicho katika chaguzi mbalimbali, Kinana alisema wamekuwa wakisimamia na kupigania haki za wananchi huku akidai kwa sasa kuna viongozi wamekuwa madalali ndani ya chama hicho.
“CCM ni chama chenye nguvu wana CCM wamekuwa wamoja na hiyo ndiyo imetufanya tumekuwa tukiendelea kuaminiwa na wananchi na sababu zipo wazi ni kusimamia na kupigania haki zao hakuna mwenye kauli wana CCM wanamuunganiko.
“Sababu nyingine ya kuendelea kuaminiwa ni uwepo wa demokrasia pana na yenye kina kwa kila mwanachama kuwa na uhuru wa mawazo kwa kusema na hata kushauri.
“Wanaoamua ndani ya chama ni wanachama wakisema ndiyo ni ndiyo na wakisema hapana ni hapana katika uchaguzi mwanachama ana haki ya kuchagua na ana uhuru wa kuchukua fomu na kugombea,’’ alisema Kinana.
Alisema kwa sasa vipo vyama vitatu pekee duniani ambavyo vinaoongoza kwa maandiko mazuri na yenye tija ambapo alivitaja vyama hivyo kuwa ni Chama cha Kikomunisti cha China, CCM na ANC cha Afrika Kusini.
Kinana alisema mwaka 2015 chama hicho kilifanya tathmini kwa miezi 12 kuanzia katika shina mpaka taifa lengo likiwa ni kupunguza urasimu na umangimeza, ambayo iliwasaidia kujua upungufu na marekebisho wanayotakiwa kufanywa.
Kuhusu suala la Serikali kuhamia Dodoma, alisema Serikali inatakiwa iungwe mkono japo alikiri kwamba mwanzo utakuwa mgumu.
Pia aliwataka wanachama wa chama hicho kuchagua viongozi wenye kazi zao katika uchaguzi mbalimbali utakaofanyika.
“Muwachague viongozi bora waadilifu wenye shughuli zao zisizotokana na CCM awe na shughuli ya kufanya,’ ’alisema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, alisema CCM kimehusika kwa asilimia kubwa katika kuleta amani na utulivu nchini huku akiponda vyama vingine kuhusika na maandamano kila kukicha.
“Hivi vingine ni vyama vya maandamano tu, amani na utulivu imeletwa na CCM kumbukeni zamani tulikuwa tunasema chuo kikuu sasa hivi tunasema vyuo vikuu Udom pekee wanamaliza wanafunzi 36,000,’’ alisema Mangula.
Maadhimisho ya miaka 40 kwa mwaka huu yamekuwa ya aina yake ambapo yamehudhuriwa na wabunge wote wa chama hicho, wakiwamo mawaziri wakuu wastaafu, John Malecela na Mizengo Pinda pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai.