Kaka wa kambo wa Kiongozi Korea Kaskazini, Kim Jong-un ameuawa nchini Malaysia huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijajulikana.
Kaka huyo wa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Nam inasemekana muda wake mwingi alikuwa akiutumia nje ya nchi yake na amekuwa akienda baadhi ya mataifa na kuisema vibaya serikali ya taifa lake ambayo inaongozwa na mdogo wake.
Polisi wa Malaysia wameuambia mtandao wa Reuters kuwa mwanaume mmoja asiyefahamika alipoteza maisha wakati akitolewa katika Uwanja wa Ndege wa Kuala akipelekwa hospitali na wakiwa njiani alipoteza maisha, huku mfanyakazi wa hospitali ya Putrajaya akisema kuwa marehemu ambaye alipokelewa jina lake la mwisho ni Kim.
Kituo kimoja cha tv cha Korea Kusini cha Chosun kimeripoti kuwa chanzo cha kifo cha Jong Nam ni wanawake wawili ambao wanahisiwa kuwa ni raia wa Korea Kaskazini ambao walimwekea sumu ambayo ilimdhuru hali iliyosababisha Jong Nam kupoteza maisha.
Kim Jong Nam na Kim Jong Un wote ni watoto wa kiongozi wa zamani wa Korea Kaskazini, Kim Jong Il, ambaye alifariki dunia mwaka 2011, lakini kila mmoja ana mama yake.