NDEGE ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q Dash 400 namba 5H TCB, juzi ilizua taharuki kwa abiria baada ya kushindwa kuruka katika uwanja ndege wa Mwanza, imefamika.
Kitendo hicho kilisababisha abiria kupiga kelele wakitaka kushushwa.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 1.00 jioni wakati ndege hiyo ikijiandaa kuruka kwenda Dar es Salaam ikiwa na abiria zaidi ya 30.
Mmoja wa abiria wa ndege hiyo, Juma Robi mkazi wa Musoma alisema ndege ilishindwa kuondoka huku ikitoa mlio tofauti ilivyo kawaida yake.
Hilo ni tukio la pili kutokea kwa ndege za shirika hilo baada ya mwezi uliopita kuruka na baada ya dakika mbili ikarejea na kutua tena katika uwanja huo.
Ilidaiwa kuwa ilitokana na kutofungwa vizuri mlango wa mizigo huku taarifa nyingine zikidai ilikuwa ni hitilafu ya kawaida.
Abiria waelezea
Mwandishi aliyefika katika uwanja huo alikuta abiria wakiwa wameshushwa huku kila mmoja akiwa anampigia ndugu yake simu kujumlisha hali ilivyokuwa.
Nao uongozi wa uwanja huo ulilazimika kuwachukua abiria wote na kuwapeleka katika hoteli kwa ajili ya chakula.
Robi akizungumza na MTANZANIA akiwa katika Hoteli ya Kigdom, alisema alifika uwanjani saa 11 jioni kwa mujibu wa tiketi yake na akapanda kwenye ndege hiyo saa 1.00.
Alisema wakati wanajiandaa kuondoka ndege ilitoa sauti ambayo si ya kawaida hali iliyosababisha abiria waangaliane kwa mshangao na hofu.
“Ilipojaribu kuisogea mbele ilishindikana maana sauti ilikuwa kubwa ya muungurumo, yaani kila mmoja alikuwa na hofu na wengine wakaanza kupiga kelele kutaka kushushwa, hali ilivyozidi tukawa hatuelewani ndipo walipoamua kutushusha na mizingo yetu.
“Walitupandisha kwenye gari lao na kutuleta mitaani kula, tumeanzia katika Hoteli ya Starmax ya Kirumba lakini hatukupata chakula.
“Tumehamishiwa hapa Kigdom na kupata chakula, wametueleza saa 6.00 tutaondoka kwenda Dar es Salaam lakini hii ni hasara maana wengine tulikuwa tumekodi nyumba, gari za kutupokea sasa sijui itakuaje.
Kauli ya ATCL
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Emmanuel Koroso, alikiri ndege hiyo kupata hitilafu wakati ikijiandaa kuruka kwenda Dar es Salaam.
“Ni kweli kuna tukio la moja ya ndege zetu kupata hitilafu wakati ikijiandaa kuruka hapa ikiwa na abiria, kilichotokea katika ndege yetu ni hitilafu ya mawasiliano baada ya kutoa indicator (viashiria) ya mfumo wa mafuta ambayo kwa namna moja au nyingine si sahihi.
“Baada ya hapo kama unavyojua ATCL ina ndege nyingine…ilikuja nyingine na kuwachukua usiku huo huo na kuwapeleka Dar es Salaam, walifika salama muda wa saa 7.00 usiku.
“Tunavyozungumza hivi tayari mafundi wamefanya utafiti wa tatizo hilo lililojitokeza na wamerusha ndege hiyo kwa majaribio hapa uwanjani wakiwa na rubani.
“Wamejiridhisha ni salama, tulichoamua ni kwmaba ndege hii irudi Dar es Salaam bila abiria iweze kupangiwa ratiba nyingine ya safari,” alisema.
Uongozi wa TAA
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Tanzania (TAA), Mkoa wa Mwanza, David Matovolwa, alisema ndege hiyo ilikuwa katika ratiba yake ya kila siku na iliwachukua abiria hao kama kawaida lakini kabla ya kuruka ikatokea kuwapo na hitilafu.
Mazoezi ya ndege hiyo
Baada ya ndege hiyo kushindwa kuruka juzi usiku, iliwekwa pembeni ya uwanja ambapo jana asubuhi ilikuwa ikifanyiwa marekebisho huku ikiwasha mara kwa mara na baadaye kuijaribisha kuruka na kutua.
Ilipofika saa 3.50 ilijaribiwa kurushwa angani ambako ilizunguka na kurejea tena saa 4:01 asubuhi. Hata hivyo ilipofika saa 4.40 iliruka kwenda Dar es Salaam ikiwa na rubani na wahandisi waliokuwa wakiifanyia uchunguzi wa tatizo lake.