Na Mussa Mbeho Katavi
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imemuhukumu mkazi wa kijiji cha Tupido Ephance Seleman (42) kutumikia miaka kifungo cha miaka minne jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na lita tisa za gongo kinyume cha sheria .
Akisoma shitaka hilo mahakamani hapo mbele ya hakaimu mfawidhi wa mahakama hiyo,Teotimus Swai Mwendesha Mashtaka wa jeshi la Polisi Baraka Hongoli alisema kuwa mshtakiwa huyo alikamatwa akiwa na sare hizo Januari , 29, mwaka huu,
Alisema siku ya tukio askari polisi walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo baada ya kupokea taarifa kuwa ni kinara wa kupika na kuuza pombe hiyo haramu ndipo walipomkuta akiwa na sare moja ya JWTZ na pombe haramu aina ya gongo lita tisa zikiwa zimehifadhiwa ndani kwake.
Mwendesha Mashtaka huyo aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi
ya mshtakiwa huyo ili iwe fundhisho kwa watu wengine ambao wamekuwa
wakimiliki sare za kijeshi kinyume cha sheria na kufanya uhalifu
wakiwa wamezivaa na kuchafua sifa ya jeshi hilo .
Aidha mshatakiwa huyo baada ya kuhojiwa alikiri kutenda
makosa hayo mawili huku akisema kuwa sare hiyo ya JWTZ alimnyang’anya mtu mmoja aliyekunywa pombe hiyo haramu nyumbani kwake na kushindwa kumlipa.
“Mheshimiwa hakimu kwanza naomba kukikiri kufanya makosa hayo lakini sare ya JWTZ nilimnyang’anya mteja wangu aliyekunywa pombe aina ya gongo iliyopikwa nyumbani kwangu baada ya kushindwa kunilipa hivyo naomba mahakama inipunguzie adhabu kwani nategemewa na familia “ alieleza
Akitoa hukumu hiyo Hakimu wa mahakama hiyo ,Teotimus Swai licha ya mshtakiwa huyo kukiri makosa yake alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili hivyo mtuhumiwa atakwenda jela miaka minne ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo .
Mwisho