SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 20 Januari 2017

T media news

Mwambusi ameiponda ratiba ya FA Cup

Na Yahaya Mohamed

BAADA ya ratiba ya mzunguko wa tano wa kombe la FA kutolewa usiku wa jana baadhi ya michezo inatarajiwa kuchezwa hapo kesho.

Miongoni ya michezo ya kesho ni ule utakao wahusisha mabingwa watetezi yanga dhidi ya Ashanti United, kuelekea mchezo huo yanga kupitia kocha wake msaidizi juma mwambusi wamelalamikia kuchelewa kutolewa kwa ratiba ya michezo hiyo.

“Kwanza nimesikitika kidogo kwa sababu tulikuwa tunajua kuwa kuna haya mashindano lakini badala ya kupata taarifa mapema tumeshindwa kupata taarifa kwa wakati.”

“Yote kwa yote kwa kuwa ratiba ilikuwa pale na sisi tuliambiwa subirini, sasa tukawa hatujui nani tutacheza nae kwa sababu mpira unahitaji maandalizi unatakiwa ujue nani utacheza nae ndio maana unaona kwenye michuano ya klabu bingwa imetoka ratiba mapema tunajua tunacheza na timu kutoka Comoro.”

“Lakini jana usiku ndio tunapata taarifa kwamba tunacheza na Ashanti lakini kwa sababu TFF ndio wanatupangia sisi hatuna shida tutacheza hiyo mechi kesho.”

“Tumetoka kwenye mashindano na tupo kwenye mashindano hatuwezi kukaa tukasema hatujajipanga lakini utaratibu ni kwamba ujue mapema unakwenda kucheza na nani ili na wewe ufanye maandalizi kulingana na mchezo husika kwa sababu kila mechi ina mahitaji yake na maandalizi yake.”

“Ni suala la kusubiri na kuona wanasababu tofauti ambazo viongozi wanazijua ndio maana hawapo leo.”

“Tunaingia kwa tahadhari hatuwezi kudharau kwa sababu bingwa wa FA ndio anawakilisha nchi kwenye kombe la shirikisho. Sasa hivi ili kushiriki mashindano ya kimataifa inabidi uwe bingwa wa VPL au FA Cup.”

Yanga na timu zote za ligi kuu zimeingia mashindanoni kuanzia mzunguko wa tano ambao unahusisha timu 32, michuano ilianza na timu 86 zikiwemo mabingwa wa mikoa, ligi daraja la pili na daraja la kwanza.