SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 26 Januari 2017

T media news

Magufuli aweka roho juu mawaziri wawili

RAIS JOHN MAGUFULI AKIENDESHA BASI LA UTOAJI HUDUMA YA YAENDAYO HARAKA (BRT) BAADA YA KUKAGUA KATIKA UZINDUZI WA MIUNDOMBINU YA MRADI WA HUO KWA AWAMU YA KWANZA JIJINI DAR ES SALAAM JANA.

RAIS John Magufuli amewaweka ‘roho juu’ mawaziri wawili baada ya kuwapa siku moja kumpelekea haraka taarifa za makusanyo ya fedha za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (BRT) tangu ulipoanzishwa.

Sambamba na hilo, Rais Magufuli amewataka mawaziri hao kumpelekea taarifa ya mradi huo kama umeleta faida ama hasara tangu kuanza kufanya kazi na kwamba hataki kusikia kitu kinachoitwa hasara.

Waliopewa maagizo hayo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa.

“Ifikapo leo jioni, hawa mawaziri wawili na viongozi wa Dart wanieleze mradi huu umetengeneza faida kiasi gani. Lazima wananchi wajue fedha wanazolipa zinakwenda serikalini au mifukoni mwa watu,” alisisitiza.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizindua awamu ya kwanza ya huduma za mradi wa BRT uliogharimu Sh. bilioni 403.5.

Alisema mawaziri hao walitoa taarifa nzuri wakati wa uzinduzi huo, lakini wamemnyima raha kitu kimoja ambacho ni kiasi cha makusanyo kilichopatikana tangu kuanza kwa mradi huo.

Mbali na kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli pia aliwaagiza mawaziri hao kuhakikisha mradi huo unapata faida na kwamba katika maisha yake yote hajawahi kusikia kitu kupata hasara.

Alisema endapo mradi huo utapata hasara, basi mawaziri hao watambue kuwa hasara hiyo haitakuwa ya serikali; bali ni ya yao.

“Haiwezekani mradi upate hasara, katika maisha yangu, sijawahi kukutana na kitu kinaitwa hasara, sasa nyie nileteeni kitu kinaitwa hasara muone,” alisisitiza Rais Magufuli.

Kadhalika, aliwaonya viongozi hao na wale wa BRT kuacha mchezo wa kuanzisha kampuni ndogo ndogo kupitia mradi huo kama vile za mafuta, kukata tiketi, na kutafuta ajira.

Rais Magufuli alisema anafahamu mchezo mchafu wote unaofanywa na viongozi wa BRT wa kujipatia fedha kwa kuanzisha kampuni ndogo ndogo kupitia mradi huo na kuwaonya waache mara moja.

MAAGIZO MENGINE

Rais Magufuli pia aliwaagiza viongozi wanaohusika na mradi huo kuhakikisha wanajenga eneo la kuegesha magari madogo eneo la Kimara Mwisho ili kuwapa nafasi watumiaji wa mradi huo kuegesha magari yao kabla ya kupanda mabasi ya mwendokasi.

Pia, aliwataka kujenga eneo la daladala katika eneo la Kimara ili kuzipa nafasi daladala kushusha abiria watakaokuwa wanatumia usafiri wa mwendo kasi.

Kadhalika, aliwataka viongozi hao kuhakikisha abiria hawatumii muda mwingi wakiwa vituoni kusubiri usafiri wa mwendokasi.

“Ipo siku nitavamia katika moja ya mabasi haya nione mambo mnayoyafanya. Nitaazima kanzu halafu nitajibanza kwenye moja ya magari hayo," alisema Rais Magufuli.

WAVAMIZI MWENDOKASI
Aidha, aliwataka askari wa usalama barabarani kuyakamata magari yanayoingia katika barabara ya magari ya mwendokasi na kuyapekeka kituoni na kutoa upepo wa matairi.

Alisema endapo askari wa usalama barabarani akiona pikipiki au chombo chochote cha moto kinatumia barabara hiyo, akikamate mara moja.

Pia, Rais Magufuli ameupa siku tano uongozi wa Jiji la Dar es Salaam na Hazina kumaliza mgogoro wa matumizi ya Sh. bilioni 3.8 zilizopatikana baada ya kuuzwa kwa hisa za kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (Uda).

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Mbarawa alisema mradi huo umetumia Sh. bilioni 403.5, huku Serikali ya Tanzania ikitoa Sh. bilioni 86.5 na Benki ya Dunia (WB) ikitoa Sh. bilioni 317.

Alisema awamu ya pili ya mradi huo itaanza eneo la Gerezani hadi Mbagala na kwamba barabara hiyo itakuwa na urefu wa kilomita 19.3.

Naye Waziri Simbachawene alisema tangu mradi huo uanze kufanya kazi umeshatoa ajira 962 na kwamba mradi huo ni wa kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na wa tatu kwa Afrika nchi ya kwanza ikiwa Nigeria na ya pili Afrika Kusini.

Alisema kwa sasa mradi huo unasafirisha abiria 200,000 kwa siku na umelenga kusafirisha abiria 450,000.

UJENZI WA RELI
Aidha, Rais Magufuli alisema serikali yake itajenga reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakayotumia mafuta na umeme.
Pia alisema itajenga reli kutoka Bandarini hadi Ruvu, lengo likiwa ni kupunguza foleni katika Jiji la Dar es Salaam.

BARABARA ZA JUU
Vile vile alisema itajenga barabara za juu maeneo ya Mwenge, Kamata, Tabata, Morocco sambamba na kutenga Sh. bilioni 38 za ujenzi wa barabara za ndani katika Jiji la Dar es Salaam.

Rais Magufuli alisema kuondoa msongamano katika Jiji la Dar es Salaam siyo hatua ya siku moja bali inahitaji muda mwingi na kuwataka wakazi wa jiji kuwa na subira.

“Ninawashangaa hawa ndugu zangu (upinzani), waliokuwa wakisema wataondoa msongamano katika Jiji la Dar es Salaam kwa siku moja wakati wa kampeni, hata daraja huwezi kujenga kwa siku moja,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Jiji la Dar es Salaam ni la biashara ambalo idadi ya wakazi wake wanaongezeka kila siku.

Alisema jiji hilo linakabiliwa na msongamano wa magari hali inayosababisha ajali, watu kuchelewa kufika kazini, upotevu wa fedha na wakati mwingine ndoa kuvunjika.

Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2013, Tanzania inapoteza Sh. bilioni 411.55 kwa mwaka kutokana na msongamano wa magari.

Alisema serikali kwa sasa ina mpango wa kujenga barabara za mpishano eneo la Ubungo na mchakato wa kumpata mkandarasi unaendelea vizuri.

Alisema kwa sasa kuna mikakati mingi ya kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa halina msongamano na kwamba serikali inashirikiana na WB na Benki ya Maendeleo ya Afrika (Afdb) kujenga barabara mbalimbali ikiwamo awamu ya pili, tatu, nne, tano na sita za BRT.

Kwa upande wake, Waziri Simbachawene alisema kwa sasa kuna upotevu wa Sh. milioni nne kwa siku katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na msongamano wa magari.