SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 4 Novemba 2016

T media news

WAZIRI MKUU ASEMA SERIKALI HAIJAFILISIKA


Waziri Mkuu Kassim Kassim Majaliwa amesema Serikali haijafilisika na kwamba mfuko wa jimbo bado unatambulika na fedha zitapelekwa kwenye majimbo na wabunge watajulishwa kiasi kilichopelekwa ili waweze kuratibu miradi yao ya maedndeleo.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Ukonga Mheshimiwa Mwita Waitara aliyetaka kupatiwa kauli ya Serikali kuhusu kutopelekwa kwa fedha za mfuko wa jimbo.

Pia Mheshimiwa Waitara alilalamikia kitendo cha jimbo lake kutengewa fedha kidogo katika mgawo wa mfuko wa jimbo ambazo ni sh. milioni 16 licha ya kuwa na wananchi wengi huku jimbo la Segerea alilosema lina watu wachache likitengewa sh. milioni 33.

Ameiomba serikali iangalie upya ugawaji huo kulingana na mazingira ya jimbo husika.

Waziri Mkuu amesema kumejitokeza matatizo kwenye halmashauri zenye majimbo zaidi ya moja na serikali inaendelea kufanya sensa kutambua idadi ya wananchi kwenye majimbo hayo ili itakapopeleka fedha iweze kuzingatia idadi hiyo na kuwawezesha wabunge kupanga miradi ya maendeleo.