Jumla ya wanafunzi hewa 65,198 wamegundulika kuwepo katika shule za msingi na sekondari nchini, ambako idadi ya wanafunzi hao isingebainika kiasi cha Sh milioni 931.3 zingepelekwa shuleni kuhudumia wanafunzi hewa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema kati ya wanafunzi hao wa shule za msingi ni 52,783 na sekondari ni 12,415.
Simbachawene alisema kazi ya uhakiki wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ilifanyika mikoa yote nchini kutokana na agizo la Ofisi ya Rais, Tamisemi kwa makatibu tawala wa mikoa yote ya Tanzania Bara.
Alisema waliagizwa kuhakiki idadi ya wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari kwa kulinganisha taarifa ilivyokuwa Machi mwaka huu wakati wa ujazaji wa madodoso ya takwimu za shule za awali, takwimu za shule za msingi, sekondari na nyaraka za mahudhurio ya wanafunzi.
Alieleza kuwa taarifa za idadi ya wanafunzi kabla ya kuhakiki Machi 2016, zilionesha kulikuwa na wanafunzi 9,746,534 wa shule za msingi na wanafunzi 1,483,872 wa shule za sekondari.
“Baada ya uhakiki tuliofanya Septemba mwaka huu, inaonesha kuwepo wanafunzi 9,690,038 wa shule za msingi na wanafunzi 1,429,314 wa shule za sekondari,” alieleza na kuongeza kuwa uchambuzi umeonesha kuwa wanafunzi 52,783 wa shule za msingi na wanafunzi 12,415 wa sekondari hawakutolewa maelezo ya uwepo wao shuleni.
Alisema kwa tafsiri rahisi hao ni wanafunzi hewa kwa shule za msingi na sekondari nchini, ambao idadi hiyo ya wanafunzi hewa kama isingebainika kwenye uhakiki huo na kupelekwa fedha, Sh milioni 931.3 zingepelekwa shuleni kuhudumia wanafunzi hewa katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Alisema kati ya fedha hizo Sh milioni 527.8 ni kwa shule za msingi na Sh milioni 403.4 ni kwa shule za sekondari.
Aliitaja mikoa inayoongoza kuwa na wanafunzi hewa ni Tabora (12,112), Ruvuma (7,743), Mwanza (7,349), Dar es Salaam (4,096), Kagera (4,763), Rukwa (4,054), Singida (3,239), Kilimanjaro (2,594), Kigoma (2,323), Njombe (2,307), Simiyu (2,081) na Arusha (1,923).
Mikoa mingine ni Mara (1,855), Tanga (1,378), Geita (1,281), Morogoro (1,172), Mtwara (882), Mbeya (786), Shinyanga (695), Songwe (512), Manyara (330), Dodoma (284), Lindi (281), Pwani (187), Iringa (161) na Katavi (0).
Waziri huyo alisema wanafunzi hewa walianza wakati serikali ilipoanza kupeleka fedha shuleni kama ruzuku.
Alisema Sh bilioni 27 zimekuwa zikipelekwa kila mwezi kama ruzuku ya uendeshaji shule za msingi na sekondari na posho ya madaraka kwa ajili ya wakuu wa shule na walimu wakuu, lakini baadhi ya walimu waliamua kuongeza idadi ya wanafunzi ili wapate fedha zaidi.
“Huu ujinga unaweza kufanywa hata katika ngazi ya wizara ni jambo la uchunguzi, zile fedha hazipiti Tamisemi zinakwenda moja kwa moja shuleni,”alieleza na kuongeza kuwa hatua za kinidhamu zinaendelea kuchukuliwa kwa wale wote waliosababisha uwepo wa wanafunzi hewa na Tamisemi inaendelea kuhakiki takwimu zilizowasilishwa.
“Serikali haitegemei tena kuwepo suala la wanafunzi hewa. Naagiza makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa na wakuu wa shule kuhakikisha suala la wanafunzi hewa halijitokezi tena katika shule zote za msingi na sekondari,” alibainisha Simbachawene.