November 25 2016 kupitia ukurasa wake wa facebook mbunge wa Nzega mjini Hussein Bashe aliamua kuandika ujumbe mrefu kwa lengo la kufikisha ujumbe wake kwa Rais John Pombe Magufuli katika utendaji kazi wake pamoja na kumpa ushauri.
‘Napenda kuchukua fursa hii kwa heshima kubwa kabisa na kwa niaba ya wananchi wenzangu wa Jimbo la Nzenga Mjini kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa uamuzi aliouchukua wa kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kumfuta kazi mwenyekiti wa Bodi hiyo‘
‘Bw. Bernard Mchomvu, kwa kutofuata maagizo ya Mhe. Rais na matakwa ya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 31 na 32 ambavyo vinaelekeza Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali kuweka fedha zao katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu.’
‘Uamuzi huo sio tu unawanufaisha walipa kodi wa Taifa letu lakini pia unakomesha tabia za matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma kwa kujitajirisha na kujinufaisha isivyo halali kwa baadhi ya Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma‘
‘Pamoja na kuwa Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Kikwete alisaini Sheria namba 5 ya Benki Kuu tarehe 7 Juni 2006 miaka takribani kumi iliyopita hakuthubutu kuchukua uamuzi mgumu na wenye manufaa kwa Taifa kama uliochukuliwa na Rais Magufuli wa kuamua kuweka fedha za mashirika ya Umma katika Akaunti Maalumu zilizopo Benki Kuu‘
‘Kutokana na uamuzi huu wa Rais Magufuli, zaidi ya Shilingi bilioni 564.6 za ikiwa ni jumla aya shilingi na fedha za kigeni katika akaunti 267 za Mashirika ya Umma na Idara za Serikali zimeokolewa zisiingie katika mikono ya ‘wapiga dili’ ambao walizoea kutumia mwanya huo kujinufaisha isivyo halali kwa fedha za walipa kodi wa Taifa letu‘
‘Katika hatua za kuendelea kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli, ninamshauri achukue hatua zaidi ya zile alizozichukua kwa iliyokuwa Bodi ya TRA, kwa kuwa mtindo wa kuweka fedha za umma katika mabenki ya biashara una harufu ya ufisadi, wizi wa fedha za umma na dalili za matumizi mabaya ya madaraka ndani ya miaka 10 iliyopita‘
‘Ni vema Mhe. Rais ikimpendeza akafikiria kuanzisha uchunguzi maalumu (forensic audit) kubaini kupitia mwanya huo wa kuweka fedha za umma kwenye benki za biashara Je Serikali ilipoteza fedha kiasi gani kwa njia ya dili chafu, na kubaini endapo kulikuwa na matumizi mabaya ya madaraka, kufunua mwanya wa kuondoa hisia na viashiria vya ufisadi, wizi na rushwa katika hatua za kuwekwa fedha hizo katika akaunti za fixed deposits‘
‘Hatua hii italisaidia Taifa kuwafikisha mbele ya mkono wa Sheria maharamia wote na wapiga dili walioliingiza Taifa letu katika hasara kubwa kwa manufaa yao wenyewe. Ikiwezekana hatua dhidi yao zichukuliwe kwa mujibu wa Sheria za uhujumu uchumi ili mahakama ya Mafisadi iliyoundwa na Mhe. Rais Magufuli ifanye kazi yake kwa kasi‘
‘Aidha, katika hatua nyingine ili kuziba kabisa mianya ya upotevu wa fedha za umma katika hatua za kudumu, ninamshauri Mhe. Rais Magufuli katika Bunge lijalo mapema mwaka 2017 apeleke Bungeni kwa hati ya dharura, marekebisho ya Sheria Namba 5 ya Benki Kuu ya mwaka 2006 ili kurekebisha vifungu vya 31 na 32 na vifungu vyake vidogo‘
‘Katika uchambuzi wangu wa Sheria hii nimebaini ipo mianya ya kisheria ambayo inaweka ulaini katika masharti ya kulazimisha Mashirika ya Umma na Idara za Serikali na Serikali za Mitaa kuweka ulinzi wa fedha za umma kwa kuzitunza katika akaunti zilizopo Benki kuu na badala yake kufungua dirisha la kuziweka fedha hizo katika benki za biashara kwa mujibu wa sheria‘
‘Kwa mfano, kifungu cha 32 cha Sheria Na. 5 ya BoT ya mwaka 2006 kinasema kuwa, ninanukuu “32.–(1) The Bank, in its capacity as a banker and fiscal agent of the Governments or of any public authority, may be the official depository of the Governments or public authority concerned and accept deposits and effect payments for the account of the Governments or public authority.” Katika taaluma ya Sheria, neno “may be”
‘Linamaanisha sio lazima kwa mujibu wa sheria kuweka fedha za Mashirika ya Umma na idara za Serikali katika akaunti za BoT. Huu ndio ulaini wa sheria ninauzungumzia ambao ulitumiwa miaka 10 iliyopita kuweka fedha za umma katika akaunti za Benki za Biashara. Ili kuweka msingi mzuri wa uamuzi wa Mhe. Rais Magufuli ni vema kifungu hiki kikabadilishwa ili kulazimisha Mashirika ya Umma kutunza fedha zao BoT kwa mujibu wa Sheria‘
‘Pia kwa kuwa juhudi za Mhe. Rais Magufuli zimeongeza ukasanyaji wa mapato kwa kodi, ninamshauri kwa kuwa sasa Serikali inaondoa zaidi ya Shilingi 1 trilion kwa mwezi kutoka kwenye mifuko ya Watanzania kwa njia ya tozo za kodi na wakati huo huo kupitia sheria tumeondoa fedha za mashirika ya Umma kutoka kwenye Mabenki ya Biashara kuna Umuhimu wa Serekali kuhakikisha Fedha zilizotengwa kwenda kwenye Miradi ya Maendeleo zinakwenda kwa kasi ili kuchochea mzunguko wa fedha kwenye Uchumi. Hatua hii itasaidia sana ku-stimulate uchumi na kupunguza mdororo unaoanza kujitokeza‘
‘Aidha pia, Namshauri Mhe. Rais kufanya marekebisho makubwa katika mfumo mzima wa uanzishaji, uendeshaji na uratibu wa biashara nchini ili kuongeza ajira nchini, kwa kuwa ripoti ya Benki ya Dunia (2016) ya kufanya biashara Tanzania (Doing Business Tanzania- 2016)‘
‘Inaonesha Tanzania kutofanya vizuri katika Sera na Sheria za usajili wa biashara mpya na mazingira ya uendeshaji wa biashara kuwa kushika nafasi ya 129 kati ya nchi 189. Kwa mujibu wa ripoti hiyo mjasiriamali akitaka kuanza biashara rasmi lazima avuke vihunzi 9 ndani ya takribani siku 26 ili aweze kufungua biashara yake! Vihunzi hivyo vinavunja moyo na kupunguza kasi ya ongezeko la ajira binafsi kwa njia ya ujasiriamali na pia inalipa Taifa hasara kwa kutokusanya kodi kutoka kwenye biashara hizi mpya kwa haraka na kwa wakati kutokana na urasimu uliopo‘
‘Pamoja na hayo pia, namshauri Mhe. Rais, agize wizara ya wiwanda na biashara na wizara ya fedha kurekebisha sheria za kodi na biashara ili kuwezesha wepesi, urahisi na uharaka wa kukusanya kodi na kuwezesha wafanyabiashara wadogo kufanya biashara kwa uhuru‘
‘Ripoti ya Doing Business Tanzania, (2016) imebainisha kuwa makampuni yanayolipa kodi huchukua saa 179 kujaza fomu za marejesho hivyo kuifanya Tanzania kuwa na utaratibu mgumu wa kulipa kodi na kushika nafasi ya 150 kati ya nchi 189 duniani kwa ugumu wa taratibu za kulipa kodi. Tukiondoa ugumu huo na kuweka wepesi, kasi ya kukusanya mapato ya kodi itaongezeka na mapato pia yataongezeka!‘
‘Kwa umahususi Serikali inaweza kuanzisha kituo kimoja cha biashara kwa wafanyabiashara wadogo (one stop business center) kitakachotoa motisha kwa kuratibu uanzishaji wa biashara husika mpaka kulipa kodi kwa njia za digitali na mifumo ya TEHAMA. Vituo hivi viwepo kuanzia ngazi ya Serikali za Mitaa ili kurahisisha shughuli za uanzishaji wa Biashara na uwekezaji kutokea chini‘
‘Marekebisho hayo ya sheria za kodi na biashara yalenge zaidi kutengeneza ‘Business Incubation’ na Misamaha ya kodi (Tax holidays) kwa wafanyabiashara wadogo wanaoanza biashara ili kusaidia kukuza biashara kuliko hali ilivyo hivi sasa ambapo biashara ndogo zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa kodi na Tozo za ushuru mbalimbali katika halmashauri zetu kwa mfano Leseni, kodi ya huduma, kodi ya mapato, na kodi za majengo‘
‘Pia kama taifa umewadia wakati Mhe. Rais awaagize BoT na Wizara ya Fedha katika kipindi cha miaka hii mitano ya awali kubadili ‘Modeli ya Uchumi’ wetu kutoka ‘Consumption module’ kwenda kwenye ‘Investment module’ na hii iendane na mabadiliko makubwa ya ‘Tax structure’ yetu na sheria za Uwekezaji na Biashara na kutengeneza motisha (Incentive package) za kisekta na si motisha za ya mwekezaji mmoja mmoja‘
‘Sekta muhimu ambazo zinahitaji kupewa kipaumbele kwenye hiyo new module ni sekta ya ngozi, na viwanda vya mazao ya kilimo‘
‘Mwisho kabisa napenda kumhakikisha Mhe. Rais kuwa mimi binafsi kama mbunge, wananchi wa Jimbo la Nzega na Watanzania wengine wote tunaoamini katika uadilifu katika ofisi za umma, tunaendelea kumuombea ulinzi kwa Mungu, na tupo nyuma yake kumuunga mkono dhidi ya vita hii ngumu ya kupambana na ‘wapiga dili’ walioligeuza Taifa letu miaka 10 iliyopita kuwa shamba la bibi‘