SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 8 Novemba 2016

T media news

Nje ya pitch: Mwaka mmoja wa Jurgen Klopp na nafasi ya kwanza EPL

Na Athumani Adam

Mwezi October 2015 Liverpool ilimtangaza rasmi kocha Mjerumani Jurgen Klopp kurithi mikoba ya Brenden Rogers. Klopp alikuwa ametoka mapumzikoni baada ya kuachana na klabu ya Borussia Dortmund ambayo aliipa mataji yote muhimu ndani ya Ujerumani.

Mbali na mataji ya ndani pia kwenye michuano ya Ulaya Dortmund chini ya Klopp ikafika fainali ambayo walipoteza dhidi ya wapinzani wao FC Bayern Munchen kwenye uwanja wa Wembley.

Ni takribani mwaka mmoja umepita tangu Klopp aingie kandarasi ya miaka mitatu kuwafundisha majogoo wa Anfield.

Miezi minne tangu alipojiunga na Liverpool, Klopp alifanikiwa  kucheza fainali ya Kombe la Ligi bahati mbaya akapoteza dhidi ya City kwa penalty 3-1. Mwezi May mwaka huu akapoteza tena fainali nyingine dhidi ya Sevilla kwenye michuano ya Europa. Kabla ya hapo Liverpool ilikuwa haijafanikiwa kutinga hatua yoyote ya fainali michuano ya Ulaya tangu mwaka 2007.

Wikiendi hii Liverpool imekaa kwenye kilele cha msimamo wa ligi kwa mara ya kwanza chini ya Jurgen Klopp. Kwenye ligi yenye Pep Guardiola, Antonio Conte, Mauricio Pochettino, Arsenal Wenger na Jose Mourinho sio jambo rahisi.

Liverpool ina wastani mzuri wa mabao hadi sasa, hakuna timu ambayo imeweza kutikisa nyavu za wapinzani mara 30 ukiondoa Liverpool. Timu inacheza soka la uhakika lenye ladha zote mabao na burudani. Pointi ishirini na sita zimetosha kumuweka Klopp kwenye nafasi ya kwanza tangu alipojiunga na Liverpool takribani mwaka mmoja uliopita.

Tofauti na msimu uliopita ambao alikuta tayari timu imesalijiliwa na Rogers, msimu huu Klopp amefanya usajili mwenyewe pia ametengeneza aina ya timu anayoitaka mwenyewe. Klopp ni miongoni mwa makocha wanaonekana kufanikiwa kimfumo kwenye msimu huu wa ligi kuu nchini Uingereza.

Ana nafasi kubwa ya kuipeleka Liverpool kwenye mafanikio mapya ya kunyakuwa taji la ligi kuu nchini humo ambalo wamelikosa kwa miaka takribani ishirini na sita.

Pep Guardiola anaonekana akipanda na kushuka akiwa na kikosi chake cha Man City. Tayari hadi sasa amepoteza pointi sita baada ya kutoka sare tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani Etihad Stadium

Jose Mourinho bado anajikongoja na kikosi chake cha Manchester United kama ilivyo kwa Mauricio Pochettino ambaye anapoteza pointi nyingi kwa kutoka sare kwenye michezo ya EPL.

Wapinzani ambao wanaweza kuzima ndoto za Klopp ni Antonio Conte ambaye amefanikiwa kuingiza mfumo wake wa kitaliano maarufu kama Catenaccio pale Chelsea.  Mwingine ni Arsene Wenger lakini kwa bahati mbaya huwa anaanza ligi vizuri na kumaliza vibaya.

Klopp anaweza kuifikisha Liverpool kwenye mafanikio ya kina Bill Shankys. Bahati nzuri Liverpool kwa sasa sio timu ambayo ina presha kubwa kuifundisha kama ilivyo kwa Manchester United au Cheslea

Huyu ni miongoni mwa makocha ambao wanaweza kukupa mafanikio kwenye timu yako tena kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha. Baada ya mwaka mmoja tangu ajiunge na Majogoo  ameshika nafasi ya kwanza kwenye ligi. Je ikifika mwezi May mwakani atakuwepo tena kwenye nafasi hiyo?  Tusubiri tuone…