Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve, amesema kwamba misikiti mingi zaidi inaweza kufungwa kufuatia hali ya dharura inayoendelea nchini humo.
Katika wiki iliyopita pekee, misikiti 4 iliweza kufungwa nchini Ufaransa huku serikali ikitoa ripoti kwa mara ya kwanza kuhusiana hatua zilizochukuliwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugaidi kuanzia mwaka 2015.
Kufuatia hatua hizo, misikiti zaidi ya 20 imeweza kufungwa ndani ya kipindi cha hali ya dharura huku sehemu kadhaa za ibada zikifanyiwa uchunguzi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Wakati huo huo, jumla ya watu 426 wametiwa mbaroni na wengine 95 wamefungwa katika magereza ya nyumbani tangu kuendeshwa kwa mashambulizi ya Paris mwaka jana.
Operesheni zimetekelezwa katika maeneo elfu 4 ambapo silaha 600 zikiwemo 77 za hatari ziliweza kutiwa mikononi.
Tangu mwanzoni mwa mwaka 2015 hadi kufikia sasa, raia 80 wa asili za mataifa ya kigeni wameondolewa nchini huku wageni wengine 201 wakiwekewa marufuku ya kuingia Ufaransa.
Watu wengine 430 wanaoshukiwa kujiunga na makundi ya kigaidi pia wamewekewa marufuku ya safari za kimataifa.
Takriban tovuti 54 zimefungwa mitandaoni na barua pepe 319 kuwekewa vizuizi kama mojawapo ya hatua za kupambana na ugaidi.
Kanuni mpya iliyowekwa tangu kutangazwa kwa ilani ya hali ya dharura nchini Ufaransa inatoa mamlaka kamili kwa wizara ya mambo ya ndani kufunga sehemu za ibada.
Ilani ya hali ya dharura ilitangazwa nchini Ufaransa baada ya kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi mjini Paris tarehe 13 Novemba 2015 ambapo watu 130 walipoteza maisha.