Profesa Anna TibaijukaALIYEWAHI kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametunukiwa tuzo baada ya kutangazwa mshindi wa mwaka 2016 wa Taasisi ya Mafanikio ya Govan Mbeki (Govan Mbeki Lifetime Achievement Award), katika sherehe iliyofanyika usiku wa kuakia jana, kwenye Ukumbi wa International Convention Center (ICC) mjini Durban, nchini Afrika Kusini.
Profesa Tibaijuka, ambaye pia alipata kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN- Habitat), ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na ufanisi aliouonyesha, ikiwa ni pamoja na kuendesha mikakati na kampeni kubwa bila kuchoka ya kupambana na makazi duni na mazingira barani Afrika na duniani, wakati akiliongoza shirika hilo.
Waziri wa Maendeleo ya Makazi wa Afrika Kusini, Lindiwe Sisulu, ndiye aliyemkabidhi tuzo hiyo na cheti Profesa Tibaijuka, baada ya kutangazwa mshindi.
Profesa Tibaijuka, ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), ametunukiwa tuzo hiyo baada ya kuonyesha kuthamini mchango wake wakati akiwa UN Habitat, kati ya mwaka 2000-2010.
Kiongozi huyo, licha ya kujipatia sifa lukuki wakati akiliongoza shirika hilo la Umoja wa Mataifa na hivyo kumuandalia njia nyepesi ya kushinda ubunge Jimbo la Muleba mwaka 2010 na hata kuteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, hata hivyo, sifa hizo zilitiwa doa baada ya kuhusishwa kwenye mgawo wa fedha tata zilizochotwa kutoka katika akaunti ya Escrow.
Profesa Tibaijuka, licha ya mara kadhaa kujitetea kwamba fedha hizo alipewa kwa ajili ya shule yake, baadhi wamekuwa wakidai kuwa kitendo hicho kimemuonyesha kuwa si mtu safi na anayestahili kuaminiwa.
Kwa maneno yake mwenyewe, Profesa Tibaijuka amekuwa akidai kuwa hayo anaonewa na kwamba hata kupokea kwake fedha hizo kumegeuzwa kuwa ni dhambi na wapinzani wake wa kisiasa.
Kutokana na hayo, wakati fulani alisikika akiunga mkono mpango wa Rais John Magufuli kuanzisha mahakama ya mafisadi.
Profesa Tibaijuka alisema chombo hicho kitachangia kutoa haki na kuweka ukweli bayana, kwakuwa watuhumiwa wengi wa ufisadi wanatolewa kafara.
Alisema akiwa kama mmoja wa wahanga wa tuhuma za ufisadi, kuanzishwa kwa mahakama hiyo kutasaidia, kwakuwa kuna kundi la watu ambalo linatolewa kafara na mafisadi ili kuficha madhambi yao.
“Ukishaanzisha mahakama ya mafisadi unatafuta haki na ukweli, Watanzania ni wepesi wepesi wa kuamini, Watanzania tuhuma tu wanaona tayari umeshakuwa convict (hatiani), mimi ni mmoja wa wahanga wa tuhuma za ufisadi na nilituhumiwa bila kuwa na uhakika, kuna mitandao ya mafisadi wenyewe wanahakikisha hawakamatwi na badala yake wanawapeleka wengine mbele ili wawatoe kafara,” alikaririwa Profesa Tibaijuka.