NAIBU Katibu Mkuu (Bara) wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kufuatilia mikutano yao ya ndani, inayoendelea sehemu mbalimbali nchini.
Mnyika alisema hayo mkoani Singida juzi akiwa kwenye moja ya mikutano ya ndani, iliyoandaliwa na Chadema kwa lengo la kuimarisha viongozi wake ngazi ya kata na wanachama ili waweze kuwafikia wananchi wa vijijini.
Naibu Katibu huyo alisema siyo jambo zuri polisi inapotumika vibaya kufuatilia mikutano ya Chadema, wakati ipo kikatiba na kuruhusiwa na serikali.
Kwa mujibu wa Mnyika, mkutano huo uliokutanisha wajumbe wa wilaya ya Ikungi, jimbo la Singida Mjini na Singida Kaskazini, ulikuwa na lengo la kuwapika viongozi wa kata ili wakaijenge Chadema imara maeneo ya vijijini.
Akizungumzia mikutano hiyo, Waziri Mkuu mstaafu wa serikali awamu ya tatu ambaye hivi sasa ni mjumbe kamati kuu ya Chadema, Fredrick Sumaye aliwataka viongozi hao wa kata kuhakikisha chama kinapata mafanikio ili hatimaye kiweze kushika dola.
Mbali ya Mnyika na Sumaye, viongozi wengine wa Chadema waliohudhuria walikuwa Mbunge Ester Matiko (Tarime Mjini), Susan Masele (Mwanza), Rose Kamili (Manyara), Jesca Kishoa (Singida) na wajumbe wengine watatu wa sekretarieti ya Chadema makao makuu.