Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akizungumza na wakazi wa Mbagala katika ziara yake ya siku kumi ndani ya jiji la Dar Es Salaam,katika kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.Katika ziara hiyo RC Paul Makonda amewataka wazazi kuchunguza muenendo wa tabia za watoto wao ili wasije wakajihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo kujiunga na vikundi vya uhalifu maarufu kama Panya Road, vinginevyo wazazi hao watachuliwa hatua za kisheria kwa uzembe wa kutokulea watoto wao katika maadili mema.
Sehemu ya umati wa Wakazi wa Mbagala na vitongoji vyake wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa Paul Makonda,alipofika kuzungumza nao na kusikiliza kero zao na hatimae kuzitafutia ufumbuzi,ambapo wakazi hao pia walipata wasaa wa kuuliza maswali ya masuala mbalimbali yanayowahusu na kuzieleza kero walizonazo katika maisha yao ya kila siku.
RC Makonda akizungumza na baadhi ya Wanafunzi wa shule ya Msingi Mbande,jijini Dar ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara yake katika wilaya ya Temeke,ambapo Paul Makonda amewataka wazazi kuwa na wajibu wa kuwasimamia na kuwachunguza watoto wao katika suala zima la kujijenga kimaadili na kuondokana ama kuepula kufanya mambo yaliyo kinyume na maadili,vinginevyo serikali itawachukulia hatua wazazi hao.
Akifafanua zaidi RC Makonda ameeleza kuwa kwa watoto wote waliochini ya umri wa miaka 18 wote kwa pamoja na wazazi wao watawajibishwa kwa mujibu wa sheria na kusisitiza kuwa anahitaji kuiona DAR MPYA ambayo kila mtanzania atakuwa na uhuru wa kufanya mambo yake bila kubughuziwa na mtu yeyote au kuhofia vitendo vya uhalifu.
Pia amewataka wanafunzi wa shule hiyo kuwa wasikivu kwa wazazi wao, walimu, viongozi wa dini na watu wote ili waweze kutimiza malengo na wajitahidi kusoma kwa bidii kwani kufanya hivyo ni kumuunga mkono Rais John Pombe Magufuli katika adhima yake ya kuboresha elimu, katika hatua nyingine RC Makonda amezindua madarasa matatu katika shule hiyo, yaliyojengwa kwa ufadhili wa Rais Magufuli.
RC Makonda akikata utepe kuashiria uzinduzi wa vyumba vya madarasa yaliyojengwa kwa fedha za Rais Dkt John Magufuli,ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,leo jijini Dar.