Ushindi wa bao 1-0 iliopata KRC Genk dhidi ya Rapid Wien unaipa nafasi timu hiyo inayotumikiwa na Mbwana Samatta kufuzu moja kwa moja hatua ya mtoano ya Europa League msimu huu.
Bao pekee la ushindi katika mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji raia wa Ugiriki Nikolaos Karelis dakika ya 11 tangu mchezo kuanza.
Nahodha wa timu ya taifa ya Taifa Stars Mbwana Samatta, aliingia uwanjani dakika ya 84 akitokea benchi kuchukua nafasi ya mfungaji wa bao Nikolaos Karelis.
Matokeo hayo yanaifanya KRC Genk kufikisha jumla ya pointi 9 baada kucheza mechi 5 za Kundi F na kuongoza kundi hilo kwa tofauti ya magoli mbele ya Athletic Bilbao ambao wanalingana kwa idadi ya pointi na mechi walizocheza.
Genk inasubiri kucheza mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi itakayoamua timu ipi itaongoza Kundi F wakati Sassuolo na Rapid Wien zenyewe zikisubiri kukamilisha ratiba kwasababu tayari zimeshatupwa nje ya mashindano hayo.