SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 8 Novemba 2016

T media news

KAFULILA AMLILIA SITTA ASEMA KUWA NI KIONGOZI WA MFANO

ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amemlilia aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa na mbunge mstaafu wa Jimbo la Urambo Mashariki mkoani Tabota, Samuel Sitta, akisema Tanzania imepoteza kiongozi wa mfano kwa vyama vyote.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kafulila alisema Sitta alikuwa ni kiongozi wa mfano kwa sababu ameacha mambo makubwa, ambayo aliyasimamia bila kutetereshwa na mtu.

“Kwa kweli naweza kusema kwamba nchi yetu imepoteza kiongozi mkubwa ambaye hakutetereshwa katika misimamo yake, ataendelea kukumbukwa katika yale mambo ambayo aliyasimamia na yatabaki kwemye kumbukumbu za watu,” alisema Kafulila.

Alisema Sitta ni mzee wake wa karibu na alimfanya kuwa sehemu ya familia yake, hata kwenye sherehe ya Jubilei ya kutimiza miaka 50 ya ndoa, alimualika kama mwanafamilia.

Aidha, alisema katika siasa, Sitta alijenga rekodi katika kusimamia anachokiamini kwa muda mrefu, jambo ambalo ni nadra sana kwa viongozi wengine na wazee wa taifa hili.

“Ndio maana alitofautiana na Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere, Sitta akafukuzwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale, lakini hakubadili msimamo wake na baadaye alirudishwa na kuchapwa viboko,” alieleza Kafulila.

Alisema Sitta alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alihutubia Bunge juu ya ufisadi, lakini Sitta akaonesha kutofautiana naye bila kuwa na woga wowote.

“Kwa hiyo huyu ni kiongozi na mzee wa mfano, alikuwa anasimamia anachoamini,” alisema Kafulila na kuongeza kuwa msiba huo ni mkubwa sana katika mioyo ya watu wanaofahamu misimamo yake na pia kwa taifa.

Alisema Bunge la Tisa aliloliongoza, alitengeneza Kanuni za Bunge ambazo zililifanya Bunge hilo kuwa lenye meno na la mfano, ambalo liliwafanya watu wapende kulifuatilia.

Kafulila aliwataka vijana kusimama katika siasa alizokuwa, akiamini Sitta kwani akiwa Spika wa Bunge, alifanya kazi vizuri na wabunge wa upande wa wapinzani kwa usawa na aliwafanya wasikilizwe pamoja na uchache wao bungeni.

“Ndio kanuni ya demokrasia, wengi waamue, lakini pia wachache wapewe nafasi ya kusikilizwa,” alisema Kafulila.