Akiwa kwenye ziara yake inayofahamika kama Dar Mpya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ametembelea makao makuu ya klabu ya Azam FC yaliyopo Chamazi wilayani Temeke.
Katika ziara hiyo Makonda amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Azam na kutaka wadau wengine kuwekeza katika uwanzishwaji wa timu.
“Nitoe wito kwa baadhi ya watu wenye uwezo waige mfano wa watu wa Azam, watengeneze timu zao, viwanja ili tuwe na watu wengi na timu nyingi zenye ushindani.”
“Hata hii migogoro ya Simba na Yanga watu wenye hela zao wasihangaike nayo, kama wamegoma kukodishwa watengeneze timu zao ili na wenyewe waendelee kunufaika kwasababu mwisho wa siku tunajua kama tuna timu nyingi kama ilivyo Azam FC ushindani utakuwa mkubwa.”
“Itafika hatua mtu anatamani acheze Azam au Simba na Yanga lakini akipima anaona kuna upande mmoja una maslahi kuliko mwingine na hivyo ndivyo tunaweza kukuza vipaji vya vijana wengi na kujenga uchumi kupoitia ajira inayotokana na michezo na mwisho wa siku tukapeperusha bendera yetu katika mataifa mbalimbali katika sekta nzima ya michezo.”
Akielezea historia ya timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2004, mtendaji mkuu wa klabu hiyo Saad Kawemba amesema, pamoja na mwendo wa kususua wa timu hiyo katika msimu huu wanatarajia kuwa na timu kamili za vijana.
“Klabu imepata mafanikio makubwa moja ni kuwa na investment yetu wenyewe kwamba mechi zetu zote za kimataifa tunacheza hapa.”
“Tuna uwezo wa kuamua kufanya mazoezi asubuhi au usiku bila kuingiliwa na mtu yeyote. Tumeanza ligi safari hii bila ya wapenzi wetu kuwa na furaha, lakini kama viongozi tunajua tumejikwaa wapi.”
“Kuanzia January 2017, Azam FC tutakuwa na senior timu, U-20, U-17 na U-15 kwahiyo huo ndio utaratibu wetu tunaokwenda nao hakuna njia ya mkato kwenye mpira inahitaji ufanye uwekezaji ndipo upate mafanikio.”