Katibu Mkuu wa klabu ya Simba Patrick Kahemele amethibitisha kuwa, kocha wa klabu hiyo Joseph Omog alihitaji golikipa mwenye uzoefu kabla ya kuanza kwa msimu huu lakini klabu hiyo ilikwama pale Mwadini Ali aliporudishwa Azam baada ya wanalambalamba kushindwana na golikipa waliyetaka kumsajili kutoka Ivory Coast.
“Mwalimu alitupa maelekezo toka mwanzo baada ya ku-train na timu wakati wa pre season. Alisema anataka golikipa mwenye uzoefu kwa sababu ya kuongeza ushindani, ila sio kwasababu magolikipa waliopa ni wabaya lakini akiwepo golikipa mzoefu ataongeza ushindani,” amesema Kahemele ambaye ni mtendaji mkuu wa klabu ya Simba.
“Tulihangaika kipindi kile kutafuta golikipa wa ndani, tukampata Mwadini Ali lakini kwa bahai mbaya akarudishwa tena Azam baada ya Azam kushindwana na golikipa wao waliyemsajili wakati huo.”
“Kwahiyo sasahivi tunachofanya ni kutafuta golikipa mwingine kwa ajili ya kusaidiana na magolikipa waliopo ili tuwe na magolikipa watatu ambao wanaubora.”
“Sehemu nyinine ambayo mwalimu ameiagiza ni ifanyiwe kazi ni sehemu ya ushambuliaji.”
Kahemele amesema kuwa, mbali na golikipa Omog anataka kusajili mshambuliaji mwenye uwezo wa kutupia kambani.
“Anataka mshambuliaji wa kusimama, washambuliaji tulionao kama Ajib ni mchezaji ambaye wakati mwingine anatumiwa kama kiungo mshambuliaji sawa na Mavugo lakini Ame Ali sio mchezaji wetu, tuponae kwa mkopo muda wowote wanaweza wakamrudisha.”