Meya wa mji wa Clay nchini Marekani, Beverly Whaling amejiuzulu wadhifa huo baada ya kuunga mkono maandishi yenye ubaguzi wa rangi kwenye facebook dhidi ya mke wa Rais Barack Obama, Michelle Obama.
Meya huyo aliingia matatani na kuamua kujiuzulu nafasi yake baada ya kuonesha kufurahishwa na ‘post’ ya kibaguzi iliyoandikwa na Mkurugenzi wa shirika moja la kutoa misaada, Pamela Taylor aliyelenga kubainisha tofauti kati ya mke wa Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump, Melania na mama Michelle Obama.
Taylor alimtusi Michelle akimfananisha na sokwe huku akimpamba Melania kuwa ni mrembo.
Meya huyo aliandika chini ya ujumbe huo wa kibaguzi, “Just made my day Pam.”
Zaidi ya watu 200,000 wamejiandikisha mtandaoni ndani ya muda mfupi kupinga ubaguzi huo na kuwataka Whaling na Taylor kujiwajibisha haraka.
Vitendo vya kibaguzi vimeripotiwa kuongezeka nchini humo tangu Trump alipotangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais.
Ingawa kauli zake wakati wa kampeni zilikuwa na matamko tata, Trump amewataka wafuasi wake kuacha mara moja vitendo vyovyote vya kibaguzi akisisitiza kuwa yeye atakuwa rais wa Wamarekani wote.