Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, SP Christopher Bageni amewasilisha maombi Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
SP Bageni alihukumiwa adhabu hiyo baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kwamba aliwaua kwa kukusudia wafanyabiashara wanne wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi mkazi wa Manzese, Dar es Salaam, katika Msitu wa Pande.
Bageni kupitia Wakili wake, Gaudioz Ishengoma, aliwasilisha maombi hayo mwishoni mwa wiki yaliyoambatana na hati ya kiapo iliyoapwa na wakili huyo.
Muwasilisha maombi anaomba mahakama hiyo kuifanyia marejeo hukumu dhidi yake iliyotolewa Septemba 13 na kusomwa Septemba 16 mwaka huu na Msajili wa Mahakama hiyo, John Kahyoza. Akitoa sababu kuomba marejeo, anadai alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa wakati wa kutathmini ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama kwa kuegemea kwenye ushahidi wa upande wa mashtaka.
Alidai katika kuchanganua ushahidi ambao uamuzi wa mahakama uliegemea, mahakama ilishughulika na ushahidi wa msingi (Exam in Chief) wa upande wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu tu ushahidi wa utetezi hususan wa Bageni au haikuutazama kabisa.Katika hati ya kiapo iliyoapwa na Wakili Ishengoma, Bageni anadai yeye na wengine wanane ambao hawako katika maombi hayo walishtakiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa makosa ya mauaji ya watu wanne katika Kesi ya jinai namba 26 ya mwaka 2006.
Bageni alikuwa mshtakiwa wa pili na katika hukumu iliyotolewa na Jaji Salum Massati, amnayo wote waliachiwa huru, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo hivyo alikata rufaa namba 358 ya mwaka 2013.Kabla ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, DPP aliwaondolea rufaa wajibu rufaa watano na kubaki wajibu rufani wanne ambao waliachiwa huru pia Septemba 16, mwaka huu.
Walioachiwa huru ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na maofisa wengine wawili baada ya mahakama kuona hakuna ushahidi wa wazi ama mazingira kuwatia hatiani.
Katika kesi ya msingi, Bageni alidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese mnamo Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande, Mbezi Luis, Dar es Salaam.