Waziri mkuu wa zamani wa Ureno, Antonio Guterres, ambaye anasubiri kuthibitishwa rasmi na nchi wanachama wa umoja wa Mataifa kuwa katibu mkuu mpya wa umoja huo, baada ya kuungwa mkono kwa asilimia 100 kutoka kwa nchi wanachama wa baraza la usalama.
Guterres ambaye ameliongoza shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na wakimbizi wa mwongo mmoja, alipata uungwaji mkono mkubwa toka kwa wajumbe wa baraza la usalama, ambapo nchi 13 kati ya 15 za baraza hilo ziliunga mkono uteuzi wake katika kura ya siri.
Wakati wa mahojiano yake, wajumbe wengi wameonesha kuridhishwa na utendaji wake ambapo hata mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kama vile Amnesty International na Human Rights Watch yamemuunga mkono.
Hii ina maanisha kuwa Guterres, atakuwa katibu mkuu mpya wa umoja wa Mataifa kuanzia mwezi January mwakani, ambapo hata nchi 5 wanachama wa kudumu na wenye kura ya turufu kwenye baraza la usalama, walipiga kura ya ndio kuunga mkono uteuzi wake.
Aliyetangaza muafaka wa nchi wanachama za baraza la usalama, alikuwa ni balozi wa Urusi kwenye umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin ambaye aliambatana na wajumbe wengine 15 wa baraza hilo, na kumtangaza Guterres kama mshindi.
Vitaly Ivanovich Churkin, balozi wa Urusi kwenye umoja wa Mataifa, ambaye alitangaza Guterres kuwa mshindi.
Baraza la usalama Alhamisi ya juma hili linaketi kuidhinisha rasmi jina lake katika kile kilichoelezwa kuwa ni kura ya wazi ambayo wanadiplomasia wengi wanasema ni utaratibu wa kawaida lakini kiujumla mwanadiplomasia huyo wa kimataifa ndiye katibu mkuu mpya.
>>>Tunamtakia ndugu Guterres kazi njema wakati atakapotekeleza majukumu yake mapya kama katibu mkuu wa umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka mitano ijayo:- Balozi Churkin.
Guterres ambaye alikuwa waziri mkuu wa Ureno kati ya mwaka 1995 na 2002, amewahi pia kushika nyadhifa kadhaa za juu, lakini kukubaliwa kwake bila kupingwa na nchi wanachama kumeonekana kuwashangaza wengi.
Waziri mkuu wa Zamani wa Ureno, Antonio Guterres, ambaye atakuwa katibu mkuu mpya wa umoja wa Mataifa.
Atakuwa katibu mkuu wa kwanza wa umoja wa Mataifa ambaye alikuwa kiongozi wa juu kwenye Serikali ya nchi yake, nafasi ambayo mara nyingi ilikuwa inakaliwa na mawaziri wa mambo ya nje.
Kulikuwa na wagombea 10 kwenye mbio hizo za kuwania ukatibu mkuu wa umoja wa Mataifa, akiwemo waziri wa mipango wa umoja wa Ulaya, Kristalina Georgieva kutoka Bulgaria ambaye aliingia kwenye mbio hizo juma lililopita.
Makamu wa rais wa zamani wa benki ya dunia, Georgieva alishindwa kupata uungwaji mkono kutoka kwa nchi 2 wanachama wa kudumu wa baraza la usalama, huku kukiwa na taarifa za ndani kuwa, Urusi ilimpinga.
Mkuu wa shirika la UNESCO Irina Bokova, ambaye alitengwa na Serikali ya Bulgaria akitakiwa kumpisha Georgieva alipata kura mbili hasi kutoka kwa nchi tano zenye kura za turufu.