SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 9 Oktoba 2016

T media news

SUMAYE Afunguka ' Kuwa Upinzani Kuna Taka Moyo Hakuna Mteremko'

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema mtu yeyote aliyepo upinzani anatakiwa kuwa mvumilivu kwa sababu katika upande huo hakuna ‘mteremko’.

Kiongozi huyo ambaye kwa sasa yupo Chadema amesema kuwa katika chama cha upinzani ni kazi kubwa inayohitaji moyo wa uvumilivu kuliko mtu aliyepo CCM.

Sumaye, ambaye aliweka rekodi ya kushikilia nafasi ya Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka 10 wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, alihamia upinzani wakati wa harakati za Uchaguzi Mkuu na kuwa mmoja wa wasemaji wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakati wa kampeni.

Akizungumza wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya Chadema wilayani Mkuranga, Sumaye amesema dola haipatikani kirahisi na kwamba inahitaji moyo wa kujitoa miongoni mwa wanachama na viongozi wao.

Tangu alipojiunga na upinzani, Sumaye amekabiliwa na misukosuko kadhaa ikiwamo kuzuiwa kuhudhuria mahafali ya umoja wa wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma Januari mwaka huu, kitendo kilichomfanya alalamikie watawala na kuonya kuwa kuwazuia wananchi kukusanyika kunaweza kusababisha madhara.

Mbali ya mwanasiasa huyo, kada mwingine wa Chadema aliyekumbana na misukosuko ya Jeshi la Polisi ni Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa ambaye aliwania urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na Ukawa.