SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 18 Oktoba 2016

T media news

Simba wapo kwenye nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa – Eddo Kumwembe

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini Eddo Kumwembe ametoa tathmini yake juu ya mwendelezo mzuri wa matokeo inayopata klabu ya Simba katika mechi zake za ligi kuu Tanzania bara (VPL) tangu kuanza kwa msimu huu ikiwa bado haijapoteza mchezo katika mechi zake 9 ilizocheza hadi sasa.

Eddo amesema ‘Wekundu wa Msimbazi’ wapo kwenye nafasi ya kutwaa taji la VPL msimu huu baada ya misimu minne mfululizo kupita wakishihudia taji hilo lienda Jangwani na Chamazi.

“Kwa mtazamo wangu nadhani Simba wapo kwenye nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa kwasababu wamesajili wachezaji wazuri. Ukiangalia wachezaji wengi wanaoisaidia Simba kwa sasa ni wachezaji wapya, kwahiyo inaonesha kwamba wamefanya usajili mzuri,” amesema Eddo alipokua akitoa maoni yake kwenye kituo cha radio juu ya mwendelezo mzuri wa matokeo ya klabu ya Simba.

“Ukiangalia mlinzi wao wa kulia (Boukungu), Mzamiru, Kichuya, Mwanjale ni wachezaji wapya walioingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja na kufanya vizuri tofauti na Simba ya misimu ya karibuni wachezaji wapya walikuwa hawaisaidii sana timu kwahiyo hiki ni kitu kizuri ambacho wamefanya.”

“Wakati mwingine unachukua ubingwa si tu kwasababu ya uwezo wako, vilevile unaombea timu nyingine kubwa zisifanye vizuri kama tulivyoona msimu uliopita kwa Leicester City, achilia mbali uhodari wao lakini timu kubwa hazikufanya vizuri kwahiyo kinachowasaidia Simba wao wanafanya vizuri lakini Yanga bado hawajakaa vizuri Azam hawapo vizuri kwahiyo wakati mwingine unaweza kuchukua ubingwa kwa uhodari wako lakini vilevile wapinzani wako kama hawako vizuri sana hawakupi changamoto kubwa.”

“Mimi nafikiri Simba wananafasi nzuri wanafanya vizuri na wanacheza mpira mzuri unavutia si kwamba wanapata matokeo ya kubahatisha. Wako vizuri kwenye ushambuliaji, wako vizuri kwenye kujilinda, wako vizuri kwenye eneo la midfield nafikiri wananafasi nzuri baada ya misimu mingi.”

Je endapo Yanga na Azam watarejea kwenye ubora wao bado Simba watakuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa wa VPL?

“Azam na Yanga hawana hati miliki ya kuchukua ubingwa isipokuwa wanaweza kuzinduka na kufanya vizuri huku Simba ikiendelea kufanya vizuri na hicho ndicho kitu tunachohitaji kwenye mpira wetu angalau tunakuwa na top three ambazo mpaka weekend ya mwisho ya kufungwa kwa msimu tunakuwa hatujajua bingwa.”

“Changamoto itakuwa kubwa hata wao wakiamka kwasababu Simba nao usitegemee kwamba watakuwa wanalala mechi tatu au mbili wanafungwa kwahiyo wanaweza wakaamka wakaikuta Simba iko mbali au imechanganya zaidi.”

Ukame wa mataji Msimbazi ulisababishwa na nini?

“Kuna wakati Simba walifanya mabadiliko kwenye kikosi chao wakaingiza wachezaji wengi sana chipukizi wakati ule wakiwa na Emanuel Okwi, alivyoondoka Okwi wale wachezaji chipukizi chini ya Ptrick Liewig wakashindwa kuchukua nafasi, walikuwepo akina Gallas, Seseme, Ramadhani Singano na wengine walishindwa kuziba mapengo wakati huo Azam na Yanga walikuwa wananunua wachezaji wenye majina makubwa.”

“Sasahivi wanawachezaji kama Kichuya, Mzamiru, Ibrahim Mohamed ambao tayari wamecheza Mtibwa na wanauzoefu labda wachezaji wao wa kigeni wa mbele Blagnon na Mavugo ambao bado hawajachanganya.”