Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya Meya Mstaafu wa Jiji la Dar es Salaam Dkt. Didas Masaburi aliyefariki dunia jana tarehe 12 Oktoba, 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema amepokea taarifa ya kifo cha Dkt. Didas Masaburi kwa mshituko na masikitiko makubwa na kwamba anaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao.
“Poleni sana familia ya Dkt. Didas Masaburi, najua huu ni wakati mgumu sana kwenu, lakini niwahakikishie kuwa sote tumeguswa sana na msiba huu kwa kuwa tumempoteza mtu muhimu, msomi mzuri, kiongozi aliyelitumikia Taifa kwa moyo wake wote na aliyesimamia kile alichokiamini”amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Aidha, Dkt. Magufuli amewapa pole wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wamempoteza Mwana CCM mwenzao pamoja na Viongozi na watumishi wa Jiji la Dar es Salaam ambao walifanya nae kazi alipokuwa Meya wa Jiji.
Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi.
“Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina” amemalizia Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
13 Oktoba, 2016