Mahakama ya Mwanzo Iringa Mjini imemuachia huru mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Kiwele baada ya kukosa ushahidi wa kumtia hatiani katika kesi ya kumtukana mwanafunzi.
Mwalimu huyo, Elizabeth Maliga (32) ameshtakiwa kwa madai ya kumtukana mwanafunzi huyo wa kidato cha sita, Rehema Mwakatobe na mama yake.
Amedaiwa kufanya kosa hilo wakati akimsainia Rehema barua ya kumuita mama yake kwenda shuleni hapo kusikiliza kosa la kuchelewa shuleni.
Hukumu hiyo imetolewa wakati Taifa likiwa kwenye mjadala mkubwa baada ya picha za video zilizosambaa mitandaoni kuonyesha kundi la walimu wa Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya likimshambulia mwanafunzi Sestian Chikungu.
Tayari Serikali imeshatangaza kuwafukuza chuo walimu hao na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo iliyochukua takriban dakika 45, Hakimu wa Mahakama hiyo, Abdallah Kutvai alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuishawishi mahakama kumtia hatiani mshtakiwa huyo.
“Jukumu la kuthibitisha kosa ni la upande wa mashtaka. Hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha tano cha Sheria ya Ushahidi ya Mahakama ya Mwanzo iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
“Mashahidi wa upande wa mashtaka wametofuatiana tarehe za kutendwa kosa hilo. Shahidi namba moja ambaye ni mlalamikaji anasema kosa limetendeka Septemba 13, mwaka huu kwenye kikao cha kujadili mwenendo wa utekelezaji wa adhabu zilizotolewa na walimu kwa wanafunzi shuleni hapo,”alisema Hakimu Kutvai.
Amefafanua kuwa shahidi namba mbili alishindwa kubainisha siku ya tukio na kutaja tarehe tatu tofauti, ambazo ni Septemba 13, 14 na 15, siku ambayo mwanafunzi huyo alipewa barua ya kurudishwa nyumbani kwao Dar es Salaam kumfuata mzazi.