Shindano la kumsaka mrembo wa Tanzania ‘Miss Tanzania 2016’ linatarajiwa kufanyika Mwanza Oktoba 28 ikiwa ni mara ya kwanza kwa shindano hilo kufanyika nje na Dar es Salaam tangu kuanzishwa kwake.
Warembo 30 watapanda jukwaani siku hiyo kutafuta mwakilishi atakayewakilisha nchi kwenye shindano la kumsaka mrembo wa dunia linalotarajiwa kufanyika Marekani Desemba mwaka huu.
Warembo hao ambao wameweka kambi kwenye hoteli ya Jozi iliyopo Msasani Dar es Salaam waliondoka jana kwenda Dodoma kwa ajili ya shindano la kusaka vipaji kabla ya kuanza ziara ya Arusha, Singida, Geita na hatimaye Mwanza kwa ajili ya fainali za shindano hilo.
Akizungumza na gazeti la Habari Leo kwenye kambi ya warembo hao jana, Mkurugenzi wa Lino International Agency ambaye ndio waandaaji wa shindano hilo, Hashim Lundenga alisema warembo hao wamefundwa kujitambua, kujiheshimu na kutokubali kurubuniwa na kujikuta wakiingia kwenye kashfa ambazo zitachafua sura nzima ya shindano hilo.
Hata hivyo, Lundenga alilia na wadhamini ambao ni changamoto kubwa wanayokutana nayo kwenye mashindano ya mwaka huu. Alisema wamepata wadhamini wachache mikoani.
Shindano hilo lilisimama takribani mwaka mmoja na nusu baada ya kufungiwa na serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa Basata kwa sababu mbalimbali za ukiukwaji wa taratibu walizojiwekea, ikiwemo udanganyifu wa umri kwa washiriki.