Na Baraka Mbolembole
MABINGWA mara mbili mfululizo wa ligi kuu Tanzania Bara watalazimika kuishinda Mtibwa Sugar siku ya Jumatano hii ili ‘kuwaziba’ midomo wale wote wanaibeza timu hiyo msimu huu.
Ndiyo, Yanga tayari wameangusha pointi 7 katika michezo 6 msimu huu lakini hupaswi kusahau kwamba kikosi cha Hans Van der Pluijm kimecheza mfululizo kwa zaidi ya miezi 24, hilo limechangia ‘uchovu’ kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Mapumziko ya takribani siku kumi pasipo kucheza mchezo wowote ni jambo zuri kuelekea game vs Mtibwa, na huku presha ikiwa juu katika mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji wa klabu, Hans na vijana wake wanapaswa kuifunga Mtibwa iliyo katika nafasi ya 3 ya msimamo.
YANGA HAIHITAJI KOCHA MWINGINE YEYOTE
Walinda mlango watatu, Deogratius Munishi, Ally Mustapha na Beno Kakolanya wananolewa vyema na golikipa bora wa zamani, Juma Pondamali.
Kwa misimu miwili sasa, Pondamali amewafanya Deo na Mustapha kujiamini na kucheza kwa viwango vya juu. Ukiachana na makosa machache katika uchezaji wa mipira iliyokufa, krosi na kona kutoka kwa Mustapha.
Dida ni kati ya magolikipa wachache waliokamilika katika soka la Tanzania. Pamoja na kuangusha pointi 7 hadi sasa, Yanga imeruhusu magoli mawili tu katika ligi na takwimu zao zinamaanisha wana safu bora ya ulinzi ambayo msingi wake ni nafasi ya golikipa.
Pondamali ni mtu sahihi zaidi katika nafasi ya kocha wa makipa kwa wakati huu na sioni sababu ya watu kumpigia chapuo Peter Manyika.
Juma Mwambusi ana hadhi ya ukocha mkuu lakini amekuwa msaidizi na mshauri mzuri wa mkufunzi mkuu wa timu hiyo, Mholland, Hans. Uwepo wa wawili hawa umechangia Yanga kushinda mataji ya FA Cup na Ligi kuu.
Ni wataalam wa mbinu na wamekuwa wakiwatumia wachezaji wenye maarifa binafsi kuwekeza mbinu zao ili timu ipate matokeo.
Mfano ni namna walivyonufaika na uwezo wa kumiliki mpira na kukimbia nao kutoka kwa mshambulizi, Donald Ngoma. Ili kushinda ubingwa wa ligi msimu uliopita Hans alihitaji kumuona Ngoma akiwasumbua walinzi wa timu pinzani na kuwalazimisha wamchezee faulo katika maeneo yao ya hatari na kuwasababia kadi nyekundu.
Ukiachana na vipaji vingi vilivyopo katika timu hiyo, Yanga imefanikiwa sana kwa sababu ya Mholland huyu na wasaidizi wake ambao si watu wa ‘jazba.’ Ni mara chache kusikia kocha huyo akiwalaumu hadharani wachezaji wake licha ya kwamba wakati mwingine wamekuwa wakicheza mchezo wa ‘kukera.’
Inawezekana wakawapo watu wanaotazama michezo mitatu ya mwisho ya timu hiyo katika ligi na kuchukulia sababu ya kusema kocha huyo si kitu.
Lakini ukitazama michezo 36 ya mwisho ya Yanga katika VPL ambayo wamepoteza mara mbili tu, michezo minne ya FA ambayo walishinda yote, michezo 6 ya Caf Champions League 2016 ambayo walipoteza mara moja, na mingine 8 ya Caf Confederation Cup 2016 ambayo walipoteza minne.
Ukijumlisha utakuta kati ya mwezi Septemba, 2015 hadi sasa, Hans ameisimamia Yanga katika michezo ya mashindano mara 54 na amepoteza game 7 tu, mechi tano akipoteza katika michuano ya Caf. Ni kielelezo tosha kwamba timu ya benchi la ufundi haina tatizo na kinachowakuta sasa ni uchovu tu wa kucheza mfululizo.
Hans alipoichukua timu hiyo mwishoni mwa Desemba, 2014 kutoka kwa Mbrazil, Marcio Maximo alianza kuifundisha katika michuano ya Mapinduzi Cup mapema Januari, 2015 na timu yake ilifika hatua ya nusu fainali, wakaingia katika ligi sambamba na michuano ya Caf 2015.
Hawakupata muda wa kupumzika wakaingia katika michuano ya Cecafa Kagame Cup 2015 ambayo walitolewa hatua ya robo fainali. Wakaanza msimu mpya wa VPL 2015/16 na hadi sasa kwa hakika kikosi chake hakijapata muda wa kupumzika.
Yanga haihitaji kocha mwingine yeyote zaidi ya Hans na timu yake ya ufundi kama kweli wanataka kuendelea kupiga hatua ndani ya uwanja.