RAIS John Magufuli amewataka watanzania kuwa mstari wa mbele, kutunza amani yao kwa kuhakikisha wanawafichua wale wote wenye lengo ya kuivuruga amani hiyo.
Pia, ametoa changamoto kwa vyombo vya habari nchini kuweka zaidi uzalendo mbele na kuandika habari za maendeleo ya nchi zinazoonekana, badala ya kung’ang’ania kuandika habari zenye mlengo wa kuiponda serikali pekee.
Rais alisema hayo mwishoni mwa wiki, wakati akizindua kiwanda cha kusindika matunda kinachomilikiwa na kampuni ya Food Products ya Bakhresa kilichopo katika Kijiji cha Mwandege wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Alisema endapo Watanzania wataichezea amani iliyopo iliyodumu kwa muda mrefu, jitihada za serikali za kuijenga nchi kiuchumi na kimaendeleo ikiwemo uchumi wa viwanda, kamwe hazitazaa matunda.
“Navipongeza vyombo vya dola kwa jitihada zake za kuhakikisha nchi inadumu kwenye amani, nawahakikishia serikali haitovumilia mtu yeyote mwenye nia ya kuivuruga amani hii,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi zinazozungumziwa kuwa uchumi wake kuwa unakua kwa kasi barani Afrika; huku uchumi wake katika robo ya pili ya mwaka pekee ukifikia asilimia 7.9.
“Lengo la serikali yangu ni kuhakikisha uchumi unakua na kufikia asilimia 7.2 lakini hadi robo ya pili ya mwaka tumefikia asilimia 7.9 tumevuka lengo. Hii ina maana kuwa mpaka tufikie robo tatu hata kama hapo katikati kutatokea mgogoro kidogo wa kiuchumi tutaweza kufikia lengo la asilimia 7.2,” alisema.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema pamoja na mafanikio hayo yanayosifiwa hadi na vyombo vya nje, hali ni tofauti hapa nchini kwani vyombo vingi vya habari vimekuwa vikiona habari za maendeleo ya nchi si habari ya kuripoti.
“Tatizo kuna Watanzania hawapendi kusifia kitu cha kwao, leo hii Dar es Salaam kuna wageni wapatao 30,000 wa madhehebu ya Bohora, sherehe yao duniani inafanyikia Tanzania, lakini huwezi kusikia vyombo vyetu vya habari zinatangaza suala hilo,” alisema Rais Magufuli.
Alisema sherehe hiyo kufanyikia nchini, ina faida kubwa kiuchumi kwa Tanzania, si tu kitaifa, bali hata kwa mtu mmoja mmoja ikiwemo kuliingizia taifa fedha za kigeni, lakini kwa kuwa suala hilo linahusu maendeleo si habari ya kuandikwa.
Pamoja na hayo, Magufuli alipongeza mwekezaji mzalendo, Said Salim Bakhresa kwa kuamua kuanzisha usafiri wa majini kutoka Dar es Salaam kwenda Mkuranga na kumhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inampa baraka zote.
Aidha, Rais alitangaza rasmi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mpango wa kupiga marufuku matumizi ya plastiki kwa kuwa zimekuwa zikiharibu mazingira.