SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 12 Oktoba 2016

T media news

Kichuya azidi kung’ara Simba ikiitandika Mbeya City Sokoine


Wekundu wa Msimbazi Simba SC wakiwa jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine kucheza na wenyeji wao Mbeya City wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Simba walionekana kuwa na dalili za kuibuka na ushindi mapema tu baada ya washambulizi wake Ibrahim Ajibu, Shiza Kichuya na Fredrick Blagnon kulisakama lango la Mbeya City mithili ya nyuki.

Iliwachukua dakika sita tu tangu filimbi ya mwamuzi ipulizwe Simba kupata bao kupitia kwa Ibrahim Ajibu ‘Fundi’, ambaye alipiga mpira wa adhabu mujarab na kutinga moja kwa moja wavuni,

Ajibu aliendelea tena kulikasakama lango la Mbeya City baada ya kuachia shuti kali dakika ya 15 lakini mpira uligonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kuokolewa na walinzi wa Mbeya City.

Simba walipata penati baada ya Blagnon kufanyiwa madhambi na kupiga mwenyewe lakini alikosa baada ya kipa wa Mbeya City kupangu mpira.

Kiungo mshambuliaji wa pembeni wa Simba aliye kwenye kiwango bora kwa sasa, Shiza Kichuya alifunga bao la pili mnamo dakika ya 33 baada ya kumhadaa beki wa Mbeya City na kuupiga mpira kwa ufundi wa hali ya juu ya kuandika bao lake la sita msimu huu akiwa ndio kinara wa mabao.