Na Baraka Mbolembole
MSHAMBULIZI raia wa Zambia, Obrey Chirwa amefanikiwa kufunga goli lake la kwanza akiwa mchezaji wa Yanga SC.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa kwa kitita cha zaidi ya milioni 200 mwezi Juni, 2016 akitokea FC Platinum ya Zimbabwe alifunga goli la uongozi dakika ya 44′ katika pambano ambalo Yanga walifanikiwa kuibuka na ushindi wa magoli 3-1 vs Mtibwa Sugar FC siku ya jana Jumatano katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
AMEIPATA FUNGUO?
Kuna wakati mshambuliaji anashikwa na ‘ukame’ wa kufunga magoli na kipindi hicho kinapomkuta ni lazima mashabiki watampigia kelele. Ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mzambia huyu ambaye licha ya kuonekana ni mzuri katika umiliki wa mpira, kutoa pasi na kuwasaidia wenzake kufunga, bado mashabiki hawakuwa wakiridhika na wengi walihitaji kumuona akifunga magoli, jukumu ambalo lilimfanya akasajiliwa katika timu hiyo ya Mtaa wa Twiga na Jangwani.
Wakati anasajiliwa mashabiki wa Yanga walikuwa na imani kubwa kwake na waliaminini mchezaji huyo angekuwa na msaada mkubwa katika upatikaji wa magoli. Chirwa hakusainiwa ili kuwa mshambuliaji wa nyongeza ambaye angetumika kama ziada ya wafungaji wa kutegemewa katika kikosi cha Hans Van der Pluijm, bali alisajiliwa kwa malengo ya kucheza sambamba na Mrundi, Amis Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma ambao kwa pamoja walifanikiwa kufunga magoli 38 katika ligi kuu msimu uliopita.
Goli lake la kwanza limewafurahisha wengi, bila shaka hata yeye mwenyewe, benchi la ufundi na wachezaji wenzake ambao wamekuwa wakimsapoti katika nyakati ngumu alizopitia.
Washambuliaji wengi huchukia wanapomaliza mechi pasipo kufunga, na inapotokea mashabiki wanapiga kelele na kukosoa thamani ya usajili wake presha huongezeka zaidi.
Goli lake vs Mtibwa alishangilia sana, na mashabiki wa timu yake walifurahi kumuona mchezaji wao ghali akifunga kwa mara ya kwanza.
Ni kama ameipata funguo yake ya kufungulia milango ya magolikipa wa timu pinzani lakini ni jambo la kuendelea kusubiri na kuona ni kipi ataendelea kufanya. Amefunga katika mechi kubwa na sasa ataenda kuwavaa Azam FC mwishoni mwa wiki akiwa tayari ameipata funguo yake.