Na MUSA MATEJA,
Risasi MCHANGANYIKO
DAR ES SALAAM: Msanii nyota wa Muziki wa Bongo Fleva mwenye mafanikio makubwa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ juzikati alinaswa usiku mnene maeneo ya Sinza Afrikasana jijini Dar akiwa na vidosho (wasichana) watatu ndani ya gari lake, Risasi Mchanganyiko lina mkanda kamili.
Ilikuwa saa 8.30 usiku
Shuhuda aliyekuwa eneo la tukio aliliambia gazeti hili kuwa, Diamond alifika mitaa hiyo mida ya saa 8.30 usiku na kupaki gari lake aina ya BMW lenye ‘plate’ namba ya jina la Platnumz, kando ya barabara karibu na sehemu ya wauza chipsi, lakini hakuna mtu yeyote aliyeshuka garini.
“Kwanza lile gari lilipopaki hakuna aliyejua kuwa ni Diamond, jamaa mmoja ndiye aliyetushitua kuwa aliye ndani ya gari ni msanii huyo baada ya kuwa ameishtukia plate namba na kwamba ndani yake kulikuwa na mademu watatu.
“Kumbe walikuwa wameagiza chipsi, upande wa ng’ambo hivi, sasa wakati wale vijana wa kihuni wanamzingira, ndipo akaja jamaa muuza chipsi ambapo dirisha la nyuma lilifunguliwa kidogo, mmoja wa wasichana waliokuwepo ndani ya gari akatoa mkono, akapokea zile chipsi na kufunga dirisha haraka kisha Diamond akaondoa gari spidi 120,” alisema mnyetishaji huyo ambaye muda wote huo alikuwa akichukua video ya tukio hilo ambapo ndani yake kunasikika sauti ya mtu ambaye hakufahamika akisema;
“Diamond, wewe unatoka na Hamisa Mabeto, ndiyo unatoka naye bwana.”
ADAI HAKULIPWA
Katika video hiyo, mara baada ya msichana huyo kupokea chipsi na gari kuondoka, mmoja wa vijana waliokuwepo eneo hilo alisikika akilalamika kuwa Diamond ameondoka na hela yake, kwani hakulipwa.
MJADALA WAIBUKA
Baada ya gari hilo kuondoka eneo hilo, vijana hao wa kihuni waliotaka kumzuia asiondoke mpaka wajue alikuwa na akina nani ndani ya gari, walianza kumjadili huku baadhi wakimtaja Hamisa Mabeto kuwa ndiye msichana anayetoka naye Diamond hivi sasa.
Aidha, wapo waliosema kuwa msanii huyo alikuwa amekwenda hapo kwa ajili ya kumchukua msichana wa kutoka naye, kwani eneo hilo ni maarufu kwa wasichana wanaojiuza.
Hata hivyo, madai hayo pia yalipingwa na baadhi yao, waliosema hatua aliyokuwa amefikia mwimbaji huyo wa Wimbo wa Salome Remix, imefikia kiwango ambacho hawezi kutafuta madada poa wa eneo hilo.
Hata hivyo, mjadala wa nani walikuwemo ndani ya gari hilo uliisha taratibu ambapo mazungumzo yaligeukia kwenye mafanikio aliyonayo msanii huyo, huku wengi wakisema kwa Bongo hakuna msanii wa muziki anayeweza kumfikia kwa sasa.
Risasi lamtafuta Diamond
Baada ya tukio hilo kunaswa live, paparazi wetu alifanya jitihada za kumsaka Diamond kupitia simu yake ya mkononi ambapo alipopatikana mahojiano yalikuwa hivi:
Risasi: Mambo vipi Diamond?
Diamond: Fresh tu, nani?
Risasi: Mwandishi wa Gazeti la Risasi hapa, kuna tukio ambalo tumelinasa, tulikuwa tunataka kupata ufafanuzi kidogo.
Diamond: Linanihusu mimi?
Risasi: Ndiyo, iko hivi, juzi Jumamosi usiku pale Afrikasana ulionekana ukiwa na wasichana kwenye gari na vijana wa kihuni wakawa wanakuzingira, hivi wale wanawake walikuwa kina nani?
Diamond: Duh! Aisee nyie ni noma, kweli siku ile nilifika pale na nilikuwa na ndugu zangu akiwemo Queen Darlin, kulikuwa wasichana watatu, tulienda pale kwa ajili ya kutafuta msosi maana tulikuwa studio, sasa wakati niko pale nikaona wale jamaa zangu wanataka nishuke, kwa hali ilivyokuwa ilikuwa ni ngumu sana kushuka ndiyo nikaamua kuondoka.
Risasi: Kuna wanaosema eti ndani alikuwepo Mobeto na mashosti zake, ni kweli?
Diamond: Hamna bwana, wale walikuwa watu wangu wa karibu tu.