WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza mkuu wa wilaya ya Mafia mkoani Pwani, Bw. Shaib Nnunduma pamoja na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Eric Mapunda kuimarisha doria kwenye eneo la bahari ili kuzuia uvuvi haramu.
Amesema vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea katika wilaya hiyo vinapaswa kudhibitiwa haraka kwa sababu vinasababisha halmashauri hiyo kukosa mapato na kushindwa kuboresha maendeleo ya wananchi.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti (Jumamosi, Septemba 24, 2016) wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Tanpesca na alipowahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kirongwe wilaya ya Mafia.
Amesema uvuvi ndiyo shughuli kuu ya uchumi na chanzo muhimu cha mapato kwa wilaya ya Mafia na suala la uvuvi haramu linaathiri sana mapato ya halmashauri hivyo ni vema wakaimarisha doria ili kukomesha vitendo hivyo.
“Lazima jambo hili lidhibitiwe. Uvuvi wa kutumia mabomu unaharibu mazingira ya chini ya bahari hivyo samaki wanashindwa kuzaliana kwa wingi. Hakikisheni watu hao wanakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuteketeza zana wanazotumia,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Alphakrust inayomiliki kiwanda cha Tanpesca, Ganeshen Vedagiri amesema kampuni hiyo imeajiri watumishi 855 kati yake 445 ni wakazi wa wilaya ya Mafia huku wanawake wakiwa 250.
Amesema wanajumla ya mabwawa 76 ya kufugia samaki aina ya kamba na kwa sasa yanayotumika ni 30 na kila moja lina uwezo wa kuzalisha kilo 5,000 katika siku siku 150 na kufanikiwa kuvuna tani 300 kwa mwaka.
Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016.2017 wanatarajia kupata wastani wa sh. bilioni 120 katika mauzo ya nje na sh. bilioni 62 kutoka katika mauzo ya ndani. Wanaltarajia kulipa kodi ya zaidi ya bilioni 15 kwa mwaka huu.
Kwa upande wake Mohamed Gomvu ambaye ni Diwani wa kata ya Kirongwe na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mafia alisema maeneo yaliyoathirika zaidi na uvuvi haramu ni vijiji vya Ndagoni (Kiega), Kifinge, Chunguruma (Tumbuju) na kisiwa cha Nyororo.
Amesema jambo linalokwamisha ukamatwaji wa uvuvi haramu ni kutokana na watumishi kukosa uamini na kuvujisha siri kwa wavuvi hao hivyo wanashindwa kuwanasa kwenye mitego yao.